ZIARA YA MHE. MUSSA RAMADHANI SIMA (MB), NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA)


ZIARA YA MHE. MUSSA RAMADHANI SIMA (MB), NAIBU WAZIRI OFISI YA
MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) KUHUSU TATHMINI YA
MAZINGIRA KATIKA MRADI WA UJENZI WA KIWANDA CHA BETRI- KIBAHA,
PWANI

Tarehe 9 Julai, 2018 nilitembelea eneo hili la uwekezaji lililopo Kibaha Mkoani Pwani
kujionea hali halisi ya uwekezaji unaofanyika katika eneo hili. Kama alivyonielekeza
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli , Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania baada ya kuniapisha, katika
kutekeleza majukumu yangu, nimefika hapa
kutembelea eneo la ujenzi wa kiwanda cha China
Boda Technical Group Ltd kitakachojishughulisha
na kurejeleza na kutengeneza Betri. Lengo la ziara
yangu katika eneo hili ni kujionea hali halisi ya
uwekezaji huu na kuhakikisha uwekezaji huu
unaendelea kufanyika bila vikwazo.
 
Napenda kuwafahamisha kwamba, wawekezaji hawa
wamekamilisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa
Mazingira na wamekabidhiwa Cheti cha E nvironmental Impact Assessment – EIA
kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kiwanda. Aidha, Katika mchakato wa EIA wa Mradi
huu kulikuwa na changamoto ya matumizi ardhi ya eneo hili na aina ya uwekezaji
unaofanyika. Baada ya kufika hapa nimejionea hali ilivyo na kwamba Mwekezaji huyu
hakupata cheti cha mazingira kwa wakati kutokana na eneo hili kuwa limetengwa kwa
viwanda vidogo na yeye anawekeza kiwanda kikubwa na kinachohusisha kemikali
hatarishi ambapo walitakiwa kubadilisha matumizi ya ardhi ili waweze kukamilisha
mchakato wa EIA. Hata hivyo, pamoja na kupatiwa cheti cha EIA, wamiliki wa kiwanda
hiki wanatakiwa kuzingatia Masharti Mahsusi yanayoambatana na Cheti hiki ambapo
pamoja na mambo mengine Mwekezaji anatakiwa kukamilisha zoezi la kubadili
matumizi ya ardhi kabla ya kuanza uzalishaji ili uwekezaji huu uendane na matumizi ya
ardhi ya eneo hili.

Kwa kuzingatia Changamoto ya matumizi ya ardhi ambayo inakabili maeneo mengi
yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini na inachangia katika kuchelewesha mchakato
wa EIA katika miradi ya ujenzi wa viwanda, napenda kutoa maelezo na maelekezo
yafuatayo yafuatayo kwa viongozi wa Mikoa, Halmashauri na Taasisi:-

Katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji
nchini hususan kwenye viwanda, baadhi ya Taasisi, Mikoa na Halmashauri nchini
zimetenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili hiyo na matumizi mengine ya
kiuchumi. Kutokana na hitaji la kisheria, maeneo yote makubwa ya uwekezaji
yanayotengwa yanatakiwa kufanyiwa Tathmini ya Mazingira Kimkakati yaani
Strategic Environmental Assessment - SEA . Hii ni kwa mujibu wa kifungu
104 na 105 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, pamoja na
Kanuni na Mwongozo ya SEA.

Hivyo, natoa wito kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri na Taasisi zote
nchini kuhakikisha kwamba wanafanya Tathmini ya Mazingira Kimkakati (SEA)
katika maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo yao. Hii
itasaidia kurahisisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira yaani
Environmental Impact Assessment – EIA kwa miradi ya uwekezaji
itakayofanyika katika maeneo hayo. Aidha, SEA itasaidia kuepusha usumbufu
unaojitokeza kutokana na baadhi ya miradi kuhitaji mabadiliko ya matumizi ya
ardhi na hivyo kuchelewesha mchakato wa EIA kama ilivyotokea kwa mradi huu.

MUSSA RAMADHANI SIMA (MB), NAIBU WAZIRI-MAZINGIRA

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments