DR NCHIMBI APIGA STOP RODE NIGHT CLUB SINGIDA



Na Nathaniel Limu
Singida jumapili julai 08,2018

MKUU wa mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi,ameagiza kufungwa mara moja  kwa ‘night klabu (jina tunalo) iliyopo jirani na shule ya msingi Ipembe mjini hapa,kwa madai inachangia kusambazwa ovyo kwa mipira ya kujamiana (kondomu) katika maeneo ya  shule hiyo.Mipira hiyo ni hatari kwa afya za wanafunzi.

Dk.Nchimbi ametoa agizo hilo leo (08/07/2018) wakati akizungumza na waumini wa kanisa la Pentekoste (FPCT) lililopo kata ya Ipembe mjini Singida.

Akifafanua,alisema night klabu hiyo imejaa vituko vingi,ikiwemo cha wasichana/wanawake kuifanya kuwa kituo chao kikuu, cha kuuza miili yao (ukahaba).

Dk.Nchimbi alisema kutokana na ukaribu wake na shule ya msingi ya Ipembe,mipira hiyo ya kondomu baada ya kutumika,inatupwa ovyo katika maeneo ya shule,ambapo ukiacha kuokotwa na wanafunzi,pia inachafua mazingira ya shule.

“Hatuwezi kuwa na night klabu au baa ambazo zinakuwa kituo cha makahaba kufanya biashara yao ya kuuza miili.Kwa mamlaka niliyo nayo,uongozi wa night klabu hiyo,usicheze na mimi.Serikali yangu inaruhusu/itaendelea kuruhusu biashara zo zote, isipokuwa zile zinazotoa fursa  makahaba  kufanya biashara yao ya kuuza miili”amesisitiza mkuu huyo wa mkoa.

Katika hatua nyingine,Dk.Nchimbi amewataka watumishi wa umma waliopo kwenye madhehebu mbalimbali ya dini,kuonyesha hofu ya Mungu wakati wakitekeleza majukumu yao.

“Watumishi wa serikali wapo kila nyumba za ibada za madhehebu mbalimbali,kwa hiyo serikali  na madhehebu ya dini yapo kwenye mnyororo moja katika kuwatumikia wananchi.Kwa hiyo nesi wakati akitekeleza majukumu yake,amtangulize mbele mwenyezi Mungu”,alisema.

Pia alisema kwa upande wa madereva wa boda boda na bajaj waumini wa madhdhebu mbalimbali ya dini,nao waonyeshe utafauti wao kwa kutii sheria za usalama barabarani bila shurti.

“Dereva wa boda boda au bajaj asiendeshe chombo chake wakati akiongea na simu,wala asitumie kilevi cha aina yo yote.Wanatakiwa waonyeshe wana hofu ya Mungu kipindi chote wawapo kazini.Kwa njia hiyo watapunguza ajali za barabarani”,alisema Dk.Nchimbi.

Kwa upande wake askofu mstaafu wa kanisa la Pentekoste,Dk. Paulo   Samwel,,alisema kanisa lake linashirikiana kwa karibu  na serikali ya awamu ya tano,katika juhudi ya kuwahimiza waumini na wasio waumini,kujiletea maendeleo endelevu.

“Serikali ya rais Dk.Magufuli,imefanya mambo mengi mazuri,tunaipongeza.Kwa hili la rais wetu kuwaita marais na majaji wastaafu ikulu kubadilishana uzoefu,ni kitendo cha kuungwa mkono na kila Mtanzania.Utamaduni huu uendelezwe kwa sababu una tija na nchi yetu”,alisema.
Aidha,Dk.Paulo,ametumia fursa hiyo,kumpongeza rais Magufuli kwa kununua ndege kubwa ambayo imetua nchini leo.Ndege  hii na zingine zilizonunuliwa chini ya uongozi wa Magufuli kwa kipindi kifupi,ni kielelezo kwamba Tanzania ya sasa kinapaa kimaendeleo.

Aidha,askofu huyo mstaafu,aliwaomba waumini wa madhehebu ya dini mkoani hapa,kumwombea kwa Mungu  mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Nchimbi,kwa madai ana maadui wengi wakiwemo wavivu na wapotoshaji.

Alisema kanisa litaendelea kuiunga mkono serikali mkoani  hapa na Tanzania kwa ujumla,katika kuhimiza na kusimamia kilimo cha korosho,alizeti na viazi vitamu.


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments