Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa
siku tatu kwa wafanyabiashara na wenye viwanda vya mafuta ya kupikia na sukari
nchini kuhakikisha bidhaa hizo zinaendelea kupatikana katika maeneo yote na
katika bei ya kawaida.
Amesema taifa hilo lina mafuta na
sukari ya kutosha na hakufai kushuhudiwa uhaba wowote.
"Natoa siku tatu kuanzia kesho
Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi mafuta yote yaliyoko bohari yaondolewe yaendelee
kusambazwa kama kawaida nchini kote ili kuondoa uhaba uliojitokeza,"
amesema Bungeni Dodoma baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw.
Charles Mwijage kutoa kauli ya Serikali kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia
nchini Tanzania.
"Kamwe Serikali haitokubali
kuchezewa na wafanyabiashara wasiowaaminifu," ameongeza.
Amesema kama uhaba wa bidhaa hiyo
utaendelea, ifikapo Jumapili Serikali itaanza kufanya msako kwenye viwanda na
maghala na kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuficha mafuta hayo.
Waziri Mkuu amesema takwimu
zinathibitisha kwamba mafuta ya kupikia yaliyoingizwa nchini humo yanatosha,
hivyo nchi haipaswi kuwa na uhaba.
0 Comments