WATU WATATU WAFUKIWA NA MACHIMBO YA MGODI SINGIDA


Kaimu kamada wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida Mayala Towo

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA

OFISI YA KAMANDA WA POLISI “M” SINGIDA
03.11.2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
(PRESS RELEASE)

AJALI YA MGODI KUPOROMOKA NA KUSABABISHA MAJERUHI

Watu watatu wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa Mkoani Singida baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo wakiwa wanachimba madini ya Dhahabu katika eneo la machimbo lijulikanalo kwa jina la ZAMBIA lililopo  katika Kitongoji na Kijiji  cha Matongo,Kata ya Mgongo, Tarafa ya Sheluhi, Wilayani  Iramba. 

Tukio hilo lilitokea siku ya tarehe 02/11/2016 majira ya saa 7:40 mchana ambapo waliofariki ni Anna d/o Martine, (56),  Paulina d/o Msengi, (45) na Magreth d/o Samwel, (45) wote Wanyiramba, Wakulima/Wachimbaji wa madini wadogo wadogo wakazi wa Kijiji cha Mgongo ambapo waliojeruhiwa ni Amri s/o Hamisi, (34)  na Sambo s/o Msengi,(16)  wote Wanyiramba, wachimbaji wadogo wadogo   na wakazi wa Mgongo ambao  wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.

Aidha Jeshi la Polisi lilipata taarifa kuhusiana na tukio hilo ambapo  askari wake walifika eneo la tukio kufanya uchunguzi wa awali na kubaini chanzo cha ajali hiyo kuwa ni wachimbaji hao kushindwa kuchukua tahadhari wakati wakifanya shughuli zao za uchimbaji.

Majeruhi wote wamelazwa katika kituo cha afya cha Mgongo na hali zao zinaendelea vizuri  ambapo miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi wa Daktari  na kukabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi.

Kuhusiana na tukio hilo hakuna mtu/watu wanaoshikiliwa ambapo Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wachimbaji kuchukua tahadhari wakiwa wanafanya shughuli za uchimbaji ambapo pia linawaomba wazazi kutoruhusu watoto wao kujihusisha na shughuli kama hizo kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 bali wawapeleke shule.









Nimashimo ya maludio ya uchimbaji ya maeneo ya kwanza kwa uchimbaji madini Tanzania ni Shelui wilaya ya Ilamba mkoani Singida


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments