Kampuni ya mchezo wa kamari nchini
Kenya, SportPesa, imesitisha udhamini wake wa michezo kutokana na uamuzi wa
serikali kuongeza ushuru hadi asilimia 35 kutoka kwa asilimia 7.5.
Akizungumza na waandishi wa habari
Jumanne, mkurugenzi mkuu na mwanzilishi wa SportPesa Ronald Karauri amesema
wamelazimika kujiondoa kwa sababu hawawezi kudhamini michezo kama watatozwa
ushuru wa asilimia 35.
Miongoni mwa michezo itakayoathiriwa
na uamuzi wa SportPesa ni kandanda, ndondi na raga.
Kwa upande wa kandanda, kampuni hiyo
hudhamini ligi kuu ya Kenya, timu za Gor Mahia, AFC Leopards na Nakuru All
Stars pamoja na ligi ya Super 8.
Kampuni hiyo ilipotangaza nia yake
mwaka jana, afisa mkuu wa KPL Jack Oguda aliambia BBC kwamba hatua hiyo itakuwa
pigo kubwa kwa soka Kenya.
Bw Karauri ameambia mwandishi wa BBC
John Nene kwamba wamejaribu kila njia kuzungumza na wakuu wa serikali lakini
hawakuelewana. Juhudi zao za mahakama kuingilia kati zimeambulia patupu.
0 Comments