SAKATA LA KUGOMBEA MAITI LILILOZUA SINTOFAHAMU SINGIDA

SAKATA la kugombea maiti lililoleta sintofahamu ya nani mwenye haki ya kuzika mwili wa marehemu,Marry Batholomew  lililodumu mjini Manyoni kwa takribani siku mbili,hatimaye limepatiwa ufumbuzi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida kutoa maamuzi ya upande wenye haki ya kuuzika mwili huo.

Msuguano wa sakata hilo kwa mujibu wa maelezo yaliyowasilishwa Mahakamani hapo,umetokana na kuwepo kwa dini tofauti kati ya familia hizo mbili,ambapo kwa upande wa mke alikuwa ni muumini wa dini ya kikristo na kwa upande wa mumewe alikuwa muumini wa dini ya kiislamu.

Hata hivyo baada ya kusikilizwa kwa msuguano huo wa pande zote mbili,yaani waweka pingamizi na wajibu maombi ya pingamizi hilo,ndipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Manyoni ikafikia maamuzi.

Akitoa maelezo Mahakamani hapo kwa upande wa madai,Wakili Msomi wa Kujitegemea,Wakili Bwana John Chigongo amedai pamoja na historia ya marehemu na vifungu mbali mbali vya sheria na katiba marehemu ameishi na mumewe kama kimada wake,kutokana na kutofunga ndoa ya maridhiano baina ya familia mbili kutokana na kutofautiana kwa imani.

Aidha Wakili huyo amedai pia kwamba awali mahari ya shilingi milioni 1.5 ilitolewa,lakini kutokana na kuvunjika kwa makubalino ya wazazi,mahari hiyo ilirejeshwa na ndipo ndoa hiyo kuahirishwa na baada ya kuarishwa ndipo marehemu aliondoka nyumbani kwao na kwenda Dar-es-Salaam kutafuta maisha na ndipo walipokutana tena na Bwana Zidiel Shabani na kuanza mahusiano yanayodaiwa ni kinyume na taratibu.

Kwa upande wake Wakili wa upande wa wajibu maombi,Bi Joyce Kalokola akiainisha vifungu vya sheria pamoja na maisha ya marehemu amedai pia kuwa marehemu alibadili dini na kuanza kuishi na mumewe kwa misingi ya imani za dini ya kiislamu.

Amedai kwamba marehemu huyo walifunga ndoa ya kiislamu ambayo kwa sasa ina miaka sita na tayari wameshazaa watoto wawili na uthibitisho wake ni cheti cha ndoa kilichosainiwa na sheikh wa Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kupewa usajili namba 60658 ,kinachoonyesha shilingi 300,000/= zilitolewa mahari kwa binti huyo kama madhehebu ya dini  hiyo yanavyoruhusu mwanamke kupanga na kupokea mahari yake.

Kwa mujibu wa Wakili Kalokola,ibara ya 19(1) ya mwaka 1977 ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyorejerewa, kuwa kila mtu ana haki na uhuru wa kuabudi imani anayoamini pasipo kuvunja sheria ya nchi.

Aidha amedai kuwa suala la kuoa na kuolewa ni makubaliano baina ya pande mbili,yaani mke na mume ilimradi tu wawe ni watu wazima, wenye akili timamu na pasipo shinikizo lolote  na kwamba wakati watu hao wakifunga ndoa,mwanamke alikuwa na umri wa miaka 25,na kwa hali hiyo alikuwa na uamuzi wake.

Akitoa maamuzi ya kesi hiyo ya madai namba 1 ya mwaka 2018, Hakimu Mfawidhi Mkazi wa Mahakama ya wilaya hiyo,Bwana Ferdinand Kiwonde amesema kwa mujibu wa sheria na kupitia vifungu vya sheria ya ndoa na katiba ni kwamba ridhaa ya wazazi itatakiwa tu endapo wanaooana hawajafikia umri wa miaka 18,lakini zaidi ya hapo ni ndoa halali.

Hakimu Kiwonde amefafanua kwamba uthibitisho wa dini kwa mujibu wa sheria ni mfumo aliokuwa akiishi marehemu ndani ya ndoa yake iliyofungwa kiislamu kama uthibitisho wa cheti cha ndoa unavyoeleza kwani aliishi kwa misingi ya kuamini dini ya kiislamu pasipo ubishi wowote.

Amesema kifungu cha 41 cha sheria ya ndoa miongoni mwa mambo yasiyobadilisha ndoa ni pamoja na mahari,hivyo kutokana na ushahidi huo ndipo Mahakama ikatoa tamko na ridhaa ya mwili huo kuzikwa kwa kuzingatia sheria,taratibu na misingi yote ya dini ya kiislamu, huku upande wa pili ukikaribishwa kushiriki zoezi hilo kwa uhuru.


Kwa upande wa familia wameshukuru Mahakama kwa kutenda haki huku Wakili,Bi Joyce Kalokola akiweka bayana kwamba kazi yao ni kuisaidia Mahakama kutenda haki na ndicho alichokifanya mwanasheria mwenzake.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments