Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa
Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) wameipongeza Mahakama Kanda ya Dodoma kwa
kuwajali watumishi ikiwa ni pamoja na kuzingatia maslahi yao.
Pongezi hizo zilitolewa na Viongozi hao
waliohudhuria katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda ya
Dodoma kilichofanyika jana tarehe 24 Aprili, 2024 mkoani Singida.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti
wa TUGHE Mkoa wa Singida, Dkt. Athuman Bunto alisema, “naipongeza sana Mahakama
kwa kuzingatia na kufuata Sheria za utumishi kwani wamezingatia maslahi ya
watumishi, sehemu kubwa ya bajeti inawagusa watumishi, mafunzo kutolewa katika
Kada zote kwa ajili ya kujengeana uwezo, hiki ni kitu kizuri.”
Aidha, amelisifu Baraza hilo kuwa, limeendeshwa kwa uwazi
watumishi wameonekana kuridhika na limekuwa shirikishi kwani hoja zilizotolewa
zilipatiwa majibu na kwa zile ambazo zilikuwa chini ya uwezo wa Kanda wajumbe
wamekubaliana kuziwasilisha katika Baraza Kuu.
Kikao hicho kiliongozwa na Mhe Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana
Masabo ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Katika Baraza hilo, taarifa za bajeti
zilisomwa kutoka Mikoa yote Miwili ya Singida na Dodoma na kuona utekelezaji
wake hususani kwenye maeneo yanayowahusu watumishi moja kwa moja na pia kuona
vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akihitimisha kikao cha Baraza hilo, Mhe.
Dkt. Masabo aliwasisitiza watumishi kuendelea kuwaelekeza na kuwasaidia wateja
wanaofika mahakamani kuhusiana na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano TEHAMA na Mifumo mbalimbali ya Mahakama kwa kuwatia moyo na kuona
mabadiliko ya TEHAMA ni msaada kwao.
Vilevile, aliwataka wajumbe wa Baraza
kuzingatia azimio la Morogoro kuhusu utunzaji wa Mazingira kwa kuendelea
kutunza mazingira na kupanda miti ya vivuli na matunda.








0 Comments