ETO JELA MIAKA KUMI


WAENDESHA MASHITAKA wamependekeza Mahakamani huko Spain kuwa Samuel Eto'oafungwe Jela Miaka 10 na kulipa Faini ya Pauni Milioni 12 kwa Udanganyifu wa Kukwepa Kodi.

Eto’o anatuhumiwa kukwepa kulipa Kodi huko Spain inayokaribia Pauni Milioni 3.2 wakati akiichezea Barcelona kati ya Mwaka 2006 na 2009.

Pamoja na Eto’o, Waendesha Mashitaka hao pia wanataka Adhabu kama hiyo ya Eto’o apewe aliekuwa Wakala wake wakati huo Jose Maria Mesalles Mata.

Hivi sasa Eto’o, Mwenye Miaka 35, anaichezea Klabuya Uturuki Antalyaspor.

Mchezaji huyo kutoka Cameroun alianza Soka lake kwenye Chuo cha Real Madrid na kisha kujiunga na Real Mallorca Mwaka 2000 na Barcelona kumchota Miaka Minne baadae ambako aliisaidia kutwaa Ubingwa wa La Liga mara 3 na UEFA CHAMPIONZ LIGI mara 2 na kisha kuondoka Mwaka 2009 kwenda Inter Milan.

Akiwa na Inter Milan, Eto’o alitwaa Ubingwa wa Ulaya Msimu wa 2009/10 chini ya Jose Mourinho.

Taarifa hizi za kutaka kusulubiwa Eto’o zimekuja Siku 1 tu baada ya Mahakama huko Spain kupendekeza Mchezaji wa Barcelona kutoka Brazil Neymar afungwe Miaka Miwili pamoja na kudungwa Faini ya Dola Milioni 10.6 kuhusiana na Kesi ya Udanganyifu wakati wa Uhamisho wake kutoka Santos ya Brazil kwenda Barcelona Mwaka 2013.

Mapema Mwaka huu, Mchezaji mwingine wa Barcelona, Lionel Messi, alishitakiwa kwa Udanganyifu na Ukwepaji Kodi huko Spain na kuhukumiwa Kufungwa Jela Miezi 21 na kulipa Faini ya Euro Milioni 1.7 lakini Kifungo hicho kikasitishwa.

Mchezaji mwingine wa Barcelona aliekumbwa na balaa kama hilo ni Javier Mascherano ambae nae alihukumiwa Jela Miezi 12 na Kifungo hicho kusitishwa.

Lakini inahofiwa kuwa kutokana na Adhabu kali ambayo Waendesha Mashitaka wanayotaka kwa Eto’o, ipo hatari kubwa Mwafrika huyo akatupwa Jela akipatikana na Hatia tofauti na yaliyowakuta Waargentina Messi na Mascherano au ambayo yatamkuta Mbrazil Neymar.


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments