Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema
Nchimbi akizungumza na wananchi waliojitokeza kupata hududma za kibingwa katika
hospitali ya Iambi ya Wilayani Mkalama.
|
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi ameagiza Kliniki
tembezi ya huduma za kibingwa kwa mkoa wa Singida kuwa endelevu huku
akizielekeza halmashauri kuandaa mpango wa utekelezaji wa zoezi hilo kwakuwa
linagusa maisha ya wananchi wa hali ya chini.
Dokta Nchimbi ametoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara
katika Hospitali ya Iambi Wilayani Mkalama ambako zoezi la kliniki tembezi ya
madaktari bingwa wa fani nane kwa Mkoa wa Singida lilikuwa linahitimishwa.
Amesema mara baada ya kukamilika kwa halmshauri zote saba mpango
wa kuanza kutoa huduma za kibingwa kwa awamu ya pili uanze mara moja kwakuwa
wagonjwa wengi walionufaika ni wale webnye kipato duni na walikuwa wameshakata
tama ya kupata matibabu.
Dokta Nchimbi ametembelea wodi ya wanawake waliofanyiwa upasuaji
na daktari bingwa wa wanawake, wodi ya akina baba waliofanyiwa upasuaji wa
magonjwa ya tezi dume na matatizo ya njia ya mkopo pamoja, ametembelea chumba
cha upasuaji wagonjwa wa macho na kumalizia wodi ya watoto waliofanyiwa
upasuaji kutokana na matatizo ya mfumo wa upumuaji na midomo sungura.
Amesema, “Ukisikiliza ushuhuda wa wagonjwa waliopatiwa matibabu
ya kibingwa utaona umuhimu wa kliniki tembezi, wengine walikwisha kata tamaa ya
kuishi na kusubiria kifo, wengine walitengwa na kusimangwa, kuna mmoja wakati
analetwa hospitali kuonana na madaktari hawa majirani waliwaambia ndugu zake
watarudisha maiti lakini amepona kabisa”.
Akitoa taarifa ya kliniki tembezi kwa Halmashauri ya
Wilaya ya Mkalama Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta John Mwombeki amesema
wagonjwa walioonwa na madaktari bingwa kwa muda wa siku nne ni 675 na
waliofanyiwa upasuaji ni 71.
Dokta Mwombeki ameeleza kuwa kliniki tembezi imekuwa na manufaa
kutokana na kuwa na gharama nafuu kuliko hospitali kubwa za rufaa ambapo
wagonjwa wengi wameshindwa kufika huko.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Injinia
Geofrey Sanga ameeleza kuwa halmashauri yake imetoa milioni 18 kufanikisha
zoezi hilo na kuahidi kuendelea kushikiana na Mkoa katika awamu ya pili ili
wananchi wote wenye uhitaji wa huduma za madaktai bingwa wazipate.
Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, madaktari bingwa
wanawake, wototo, macho, upasuaji, mifupa na njia ya mkojo wametoa huduma za
kibingwa wilayani Mkalama kuanzia Februari 27 hadi Machi 3.
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Singida amezindua rasmi kilimo cha
korosho kwa kushiriki zoezi la upandaji wa mikorosho na mihogo na kuhamasisha
wananchi kupanda mikorosho hasa katika mashamba yao waliyolima mihogo.
Dokta Nchimbi amesema korosho ni zao linaloweza kuvunwa kwa
zaidi ya miaka hamsini na pia ni rafiki wa mazingira, huku akiendelea
kusisitiza kilimo cha viazi lishe kwakuwa ni mkombozi wa uchumi wa wananchi wa
Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipanda Mkorosho katika shamba la Mkulima wa kijiji cha Gumanga wilayani Mkalama kama hamasa kwa wananchi wengine wapande zao hilo.
|
Wananchi wa kijiji cha Nkungi na watendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakisaidiana kupanda viazi lishe katika shamba la Mkulima ili kuhamasisha kilimo hicho.
0 Comments