KATIKA mtazamo tofauti jamii ya Kinyaturu Vijana wanne wa kijiji
cha Msungua Kata ya Sepuka wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida kwa pamoja walimla
nyoka mwenye sumu jamii ya Koboko mwenye uzito wa kilo 2 na urefu mita moja,
mmoja kati yao kuzidiwa hadi kunyweshwa maziwa na wazazi wake na kupelekwa
zahanati kuchunguzwa.
Akitoa maelezo kwa gazeti hili juzi katika eneo husika
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Iporyo Saidi Ngimba amesema vijana hao walimkuta
nyoka huyo mwenye urefu wa mita moja kwenye mikorosho na kumchukua nyoka huyo
akiwa mzima hadi kwenye migahawa.
Saidi amesema vijana hao walimchukua nyoka huyo kwa nia
ya kutaka kumla kwa kumchoma kwa moto hivyo walifika kwenye migahawa vibandani
kufanya shughuli hio, amewataja vijana hao kuwa ni Msanya Ramadhani Mwela,
Rajabu Omari, Ramadhani juma na Ntunda Sima.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja wa
wale vijana Ramadhani Juma amesema ni kweli wamemla nyoka huyo na walimkuta
kwenye mikorosho wakamkamata wakamchukua mzima hadi mabandani wakapewa
jiko, mkaa, moto, chumvi na pilipili wakamkata kichwa na mkia.
Juma ameendelea kusema wakamchuna ngozi, wakamtoa mrija wa
sumu wakampaka chumvi na pilipili wakambanika na alipokauka vizuri wakaanza
kumla kila mtu ananyofoa sehemu anayotaka lakini baadae jioni yake mwenzao
Ntunda Sima alianza kulewa akazidiwa akanyweshwa maziwa lita moja na baadae
alipelekwa zahanati ya Msungua kuchunguzwa na tiba na hiyo ni kwa sababu
alikula nyama ya kwenye mkia wa nyoka huyo.
Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Msungua Omari
Bayyu (CCM) baada ya kupata taarifa hizo amemuagiza Mwenyekiti wa Kitongoji cha
Iporyo walipo vijana hao kuwa karibu nao ili kuratibu afya zao na kama itatokea
mabadiliko kwenye miili yao wakimbizwe haraka vituo vya afya na Hospitali kubwa
kwa Uchunguzi na tiba hata hivyo kabila la Wanyaturu ni mwiko kula nyoka na si
Utamaduni wao.
Mwisho.
0 Comments