Raisi Magufuli katika ziara ya kanda ya ziwa |
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli,
ameyaonya magazeti mawili ambayo amesema yanaandika habari za uchochezi na
kupotosha wananchi.
Amesema hatua ya magazeti hayo inahatarisha amani nchini humo.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akikagua na kufungua kiwanda
cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga kaskazini magharibi
mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu, kiongozi huyo amesema
serikali haitayavumilia magazeti hayo mawili akisema yanaweza kuhatarisha amani
ya nchi kama ilivyotokea katika nchini jirani ya Rwanda na kupelekea mauaji ya
kimbari nchini humo.
''Serikali ya kutumbua majipu haiwezi kuacha kutumbua magazeti
yanayofanya mambo ya uchochezi hatuwezi kuiacha Tanzania ikawa dampo la eneo la
kuweka maneno ya uchochezi chini ya utawala wangu," alisema Dkt Magufuli.
"Hilo halitakuwepo kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao
ni kuchochea tu ikizungumzwa habari hii wao wanageuza hii nasema na nataka
wanisikie siku zao zimeshafika kama wanasikia wasikie wasiposikia wasisikie
lakini magazeti mengine na vyombo vyote vingine vinatoa uchambuzi mzuri sana''.
Rais Magufuli amekuwa akikosolewa na baadhi ya wadau kwa tuhuma
kwamba anakandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Baraza la Habari nchini Tanzania tayari limewasilisha kesi
mahakamani kupinga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari iliyopitishwa na bunge
la nchi hiyo Novemba mwaka jana na siku chache baadaye ikatiwa saini na Rais
Magufuli.
Mwishoni mwa mwaka jana, mwanzilishi wa mtandao wa Jamii Forums
Maxence Melo alikamatwa na kushtakiwa kwa kukataa kufichua maelezo kuhusu watu
wanaochangia kwenye mtandao huo.
Aliachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa takriban wiki moja.
0 Comments