MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Ajibu ambaye yupo nchini Misri akifanya
majaribio katika timu ya Haras El Hodood Jumamosi alifanya vipimo vya
awali vya afya na kufuzu na sasa yupo kwenye mtihani wa pili wa kutazamwa uwezo
wake uwanjani.
Ajibu aliondoka nchini Ijumaa wiki iliyopita ambapo atafanya majaribio ya
siku 10 na kwamba akifuzu majaribio hayo basi atarejea nchini kuendelea na
taratibu zingine ikiwemo viongozi wa Simba kumalizana na timu hiyo.
Ajibu amesema kuwa anaamini atafanikiwa kwani kila kitu kinakwenda vizuri
na kwamba akimaliza majaribio hayo atarejea nyumbani kumalizia mkataba wake na
Simba uliobaki miezi sita.
"Kila kitu kinakwenda vizuri na vipimo kabla ya kuanza majaribio
nilifanya na vipo vizuri, Mungu akipenda nitamaliza majaribio yangu mwisho mwa
wiki na nitarejea nyumbani kwani bado nina mkataba na Simba," alisema
Ajibu.
Ajibu ambaye msimu
uliopita alikwenda kufanya majaribio Afrika Kusini lakini dili lake lilikwama
kwani alibakiza mkataba wa mwaka mmoja Msimbazi na sasa hajasaini mkataba mpya
lengo lake ni kwenda kucheza nje akiwa mchezaji huru.
0 Comments