Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa msaada wa Dola za Marekani elf 50,000 takribani milioni 108 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mwezi Septemba 2016.
Msaada huo
ulikabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe.
Song Geum Young na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki,
Dkt. Augustine Mahiga (Mb) kwa niaba ya Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).
Baada ya
kupokea msaada huo, Dkt. Mahiga aliishukuru Serikali ya Korea na kuahidi kuwa
msaada huo ataukabidhi kwa Mhe. Waziri Mkuu ili uweze kutumika kama ulivyokusudiwa.
Mhe.
Mahiga alisema kuwa Korea imekuwa mbia mkubwa wa Tanzania tokea nchi hiyo
ilipoanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Tanznaia miaka 25 iliyopita. Alieleza
kuwa katika kipindi hicho Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ya
kiuchumi, kijamii na ya kibinadamu ukiwemo huu wa leo ulioelekezwa kwa
waathirika wa tetemeko la ardhi la mkoani Kagera.
Mhe.
Waziri alitaja misaada ambayo Korea imeipatia Tanzania ni pamoja na ujenzi wa
daraja la Malagarasi mkoani Kigoma, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Mloganzila
na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya ya Mama iliyopo Chanika. Aidha,
Korea hivi karibuni itaanza ujenzi wa daraja la Selander ambalo linatarajiwa
kuanzia ufukwe wa Coco, Oysterbay hadi maeneo ya hospitali ya Aga Khan, Upanga
jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mahiga alibainisha pia kuwa Jamhuri ya Korea itatoa msaada mkubwa zaidi wa
maendeleo kwa Tanzania kuliko nchi yeyote ya Afrika. Taarifa hiyo ilitolewa na
Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se alipofanya naye mazungumzo
kando ya Mkutano wa nchi za Afrika na Korea uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia
tarehe 06 na 07 Desemba 2016.
Kwa upande
wake, Balozi wa Korea nchini aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na
Tanzania hususan kutoa atia misaada ya maendeleo ili iweze kutimiza azima ya
Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Desemba 2016.
0 Comments