WALIMU NA WAZAZI SEPUKA WAPONGEZWA KWA KUONGEZA UFAULU WA WANAFUNZI

                                        

                                                                     picha kutoka maktaba 

SINGIDA -IKUNGI

NA Mwandishi  wetu

Afisa Mtendaji wa Kata (WEO) ya Sepuka, wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Bahati Mkungile, amewapongeza walimu na wazazi wa kata hiyo kwa jitihada kubwa walizozifanya katika kuinua kiwango cha elimu na kuhakikisha wanafunzi wanafaulu masomo yao.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya wanafunzi 354 kutoka shule tano za msingi za Musimi, Italala, Mnang`ana, Safina na Njaa kufaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2025 na kuanza masomo ya Kidato cha Kwanza mwaka 2026 katika shule za sekondari za Msungua na Sepuka.

Bahati Mkungile amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wazazi na viongozi wa Serikali kutoka vijiji vya Musimi, Msungua na Mnang`ana, ambavyo ndivyo vinamiliki shule hizo za msingi. Ameeleza kuwa ushirikiano huo umejenga mazingira bora ya kujifunza na kuongeza hamasa kwa wanafunzi kuelewa umuhimu wa elimu.

Akizungumza ofisini kwake, Bahati alisema ongezeko la ufaulu ni matokeo ya bidii ya walimu darasani, usimamizi wa karibu kutoka kwa wazazi pamoja na juhudi binafsi za wanafunzi katika masomo yao.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata ya Sepuka, Iddi Kisuda, amesema jitihada hizo zimezaa matokeo yanayohitajika na Taifa. Ameongeza kuwa endapo wazazi wataendelea kushirikiana kikamilifu na walimu mwaka 2026, ufaulu utaongezeka zaidi kuliko mwaka uliopita.

Kisuda pia ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya elimu kupitia ajira za walimu wenye sifa, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule pamoja na ujenzi wa nyumba bora za walimu.

Akitoa taarifa ya mapokezi ya wanafunzi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Msungua, Nossiah Bembela, amesema shule hiyo tayari imepokea wanafunzi 185, huku 29 bado hawajaripoti. Amewahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanafika shuleni kwa wakati.

Naye Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sepuka, Mwalimu Abubakari Amasi, amesema shule yake imepokea wanafunzi 105, huku 35 wakitarajiwa kuripoti. Amehimiza wazazi kuzingatia muda na taratibu za kuanza masomo.

Mkazi wa Kijiji cha Msungua, Ramadhani Shabani Kiteu, amesema ufaulu huo umetokana na jitihada za walimu kupitia kambi za masomo, kuongeza muda na siku za ufundishaji kwa wanafunzi wa darasa la saba kwa kushirikiana na wazazi.



Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments