WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (pichani) amepeleka rasmi katika Kamati ya Bunge
ya huduma na maendeleo ya jamii, maombi ya kutaka Bunge kuruhusu wabunge wanaume
kuvaa mashati ya vitenge, batiki na nyinginezo za asili ndani ya Bunge.
Hatua hiyo itaondoa sheria ya wabunge
wanaume kuvaa suti, jambo linalowafanya kupata shida pale vipoza upepo
vinaposhindwa kufanya kazi.
Mwakyembe alisema hayo wakati wa
maadhimisho ya siku ya sanaa na utamaduni iliyoadhimishwa ndani ya uwanja wa
Maonesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) yanayofanyika katika viwanja vya
Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa suala hilo likipitishwa
na Bunge, litachochea kuongeza utengenezaji wa mavazi hayo pamoja na
wajasiriamali kuwa wabunifu zaidi.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba
na uvaaji wa mavazi yenye rangi za taifa, hivyo maombi yakipelekwa na
kukubalika yatachochea sanaa nchini.
Dk Mwakyembe alisema kazi za sanaa na
utamaduni katika maonesho ni fursa ya wanasanaa kuonesha ubunifu na vipaji
walivyonavyo huku akibainisha siku kama hiyo mwakani wataitangaza zaidi ili
kupata washiriki kutoka nchi nzima.
Alisema tamasha kubwa la sanaa katika
nchi za Afrika Mashariki linalotarajiwa kufanyika Septemba au Oktoba mwakani,
litafanyika katika viwanja hivyo, wataanza kujipanga ili kuangalia namna
watakavyofanya kutokana na ukubwa wa uwanja huo.
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Stella Manyanya alisema maonesho ya mwaka huu yamefana katika sanaa kwani
zamani watu walikuwa wanakusanya vya nje ya nchi na kuuza lakini sasa nyingi
zimetengenezwa na watanzania wenyewe.
Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania
(TANTRADE), Edwin Rutageruka alisema wameamua kuwa na siku hiyo kwa ajili ya
kutangaza sanaa za Tanzania huku akitaka wanautamaduni na wadau wa sanaa
kutumia uwanja huo kwa shughuli mbalimbali.
0 Comments