CCM YATEKELEZA AHADI YA KUTATUA KERO ZA WANANCHI – MGHONTO

 





SINGIDA

Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki, Mhe. Thomas Mghonto (Chief), ametembelea na kujionea zoezi la kliniki ya msaada wa kisheria lililozinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, katika viwanja vya Ukumbi wa RC Mission, Manispaa ya Singida.

Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Mghonto alimpongeza Waziri Dkt. Homera kwa uamuzi wa kufika mkoani Singida na kuleta huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi, akieleza kuwa ukosefu wa elimu ya sheria umekuwa changamoto na kero kubwa kwa wananchi wengi, hususan wale wa kipato cha chini.

Mbunge huyo alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakipoteza haki zao kutokana na kutokujua misingi ya kisheria, hivyo kliniki hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi kupata msaada, ushauri na elimu ya sheria bila gharama.

Aidha, Mhe. Mghonto alisisitiza kuwa zoezi hilo ni utekelezaji wa moja ya ahadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa kwa vitendo, huku akibainisha kuwa upatikanaji wa haki ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera,akizindua kliniki hiyo katika siku hiyo alisema kuwa lengo la kliniki ya msaada wa kisheria ni kuwasaidia wananchi kupata haki zao kwa urahisi, pamoja na kuwajengea uelewa kuhusu haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria za nchi.

Dkt. Homera aliongeza kuwa serikali itaendelea kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki bila vikwazo vya gharama au umbali.

Kliniki hiyo imepokelewa kwa furaha na wananchi wa Singida, wengi wao wakieleza kuwa huduma hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi na masuala mengine ya kisheria yanayowakabili katika maisha ya kila siku.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments