MWANZA
Na Mwadishi wetu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu
Nchemba, amewaagiza watendaji wa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokozi cha
Kikanda – Mwanza kuhakikisha kituo hicho kinaendeshwa kwa saa 24 kwa siku na
kwa ufanisi wa hali ya juu, ili kutoa huduma za haraka na zenye tija kwa
wananchi.
Dkt. Mwigulu ametoa maagizo hayo leo Januari 23, 2026, mara
baada ya kutembelea kituo hicho kilichopo jijini Mwanza, ambacho kimegharimu
takribani shilingi bilioni 19.8 kujengwa.
Amesisitiza kuwa huduma za utafutaji na uokozi ni huduma
nyeti zinazolenga kuokoa maisha ya watu, hivyo Serikali haitavumilia uzembe,
kusinzia kazini au ucheleweshaji wa utoaji wa msaada pale unapohitajika.
“Hii ni kazi ya kuokoa maisha. Uzembe, kusinzia au
kuchelewesha kutoa msaada ni kuhatarisha maisha ya Watanzania. Kituo hiki
lazima kifanye kazi saa 24,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho ni
uthibitisho wa dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto
mbalimbali zinazowakabili, hususan katika sekta ya usalama na uokozi
Ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa kituo hicho ulipangwa kutekelezwa kati ya mwaka 2018 hadi 2020, lakini ulisimama baada ya baadhi ya washirika kujitoa. Hata hivyo, Rais Dkt. Samia alielekeza kituo hicho kijengwe kwa kutumia fedha za ndani, ili kuhakikisha hususan wavuvi na wananchi wengine wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya maji wanapata huduma za usalama kwa wakati.







0 Comments