WAZIRI MKUU
DODOMA
Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Dkt. Mwigulu Nchemba, ameshiriki katika zoezi la upandaji miti lililofanyika
mbele ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma.
Zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za kumuunga mkono Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia
uamuzi wake wa kizalendo wa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa vitendo
vinavyolenga kulinda na kuhifadhi mazingira.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu,
akiwa ameambatana na mwenza wake Mama Neema Mwigulu, alimpongeza Rais Dkt.
Samia kwa uongozi wake thabiti unaoendelea kudhihirisha maono, ubunifu na
dhamira ya kulinda maslahi mapana ya Taifa.
Alisema kuwa zoezi hilo limeleta utofauti mkubwa kwa
kuchochea upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali nchini, akibainisha kuwa
katika vitabu vitukufu, kupanda mti ni miongoni mwa ibada kutokana na manufaa
makubwa yanayowafikia watu wengi.
Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwahimiza Watanzania kuiga
mfano huo kwa kuadhimisha siku zao za kuzaliwa kwa kupanda miti. Alisisitiza
kuwa nyakati za kumbukumbu kama hizo zitumike kufanya matendo yenye kuacha
alama chanya na manufaa kwa jamii.
Katika zoezi hilo, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipanda mti wa aina ya MDODOMA/MTIMAJI (Trichilia emetica).







0 Comments