SINGIDA
Serikali imesema utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa
Kisheria nchini umeendelea kuleta mafanikio makubwa, ambapo hadi sasa wananchi
zaidi ya milioni tatu wamefikiwa na kupatiwa elimu ya msaada wa kisheria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki ya siku mbili ya
kampeni ya elimu ya kisheria mjini Singida, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.
Juma Homera, amesema kati ya wananchi waliopata elimu hiyo, wanaume zaidi ya
milioni moja na wanawake zaidi ya idadi hiyo wamefikiwa, hatua inayolenga
kuhakikisha wananchi wanazifahamu na kuzitetea haki zao za msingi.
Waziri amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa
awamu ya kwanza ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuimarisha
haki za binadamu, utawala bora na upatikanaji wa haki kwa wananchi wote.
Uzinduzi wa kliniki hiyo umefanyika katika ukumbi wa Kanisa
la Roman Katoliki mjini Singida, ambapo Waziri ameambatana na wataalamu kutoka
Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Naibu Waziri wa wizara hiyo.
Aidha, Dkt. Homera amesema elimu hiyo ni endelevu na
imelenga kuhakikisha wananchi wanapata haki zao bila vikwazo. Katika mkutano
huo, Waziri alipata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kutoa
maelekezo kwa wataalamu ili kuzifanyia kazi.
Katika ziara yake mkoani Singida, Waziri pia amefanya vikao
vya ndani katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, akikutana na wakuu wa wilaya na
wakurugenzi. Sambamba na hilo, ametembelea Gereza la Mkoa wa Singida pamoja na
kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Mahakama Kuu ya Mkoa wa Singida.







0 Comments