WIZARA YA MAMBO YA NDANI BINGWA WA MPIRA WA WAVU





Huu ni Mchezo wa fainali baina ya Mambo ya ndani Dhidi ya Tanesco

                          Mchezo mshindi wa tatu baina ya Dodoma JIJI na TRA huku TRA wa kiibuka kidedea.

Na Cales katemana, Singida

Timu ya wanaume ya mpira wa wavu ya Wizara ya Mambo ya Ndani imeibuka mabingwa wa michuano ya Kombe la Mei Mosi, huku nahodha wao akisema mashindano ya mwaka huu yalikuwa na ushindani mkali.

Katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Chuo cha Uhasibu mkoani Singida, timu hiyo iliibuka na ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa matokeo ya (25-20, 25-19 na 25-22).

Nahodha wa timu hiyo, Dismas Amini, amesema licha ya kikosi chao kuundwa na wachezaji kutoka vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama kama Magereza, Polisi, Uhamiaji pamoja na Zimamoto na Uokoaji, walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa timu nyingine.

"Timu nyingi mwaka huu zimekuja zikiwa na viwango vya juu na makocha waliobobea, hali iliyofanya mashindano kuwa magumu zaidi kuliko mwaka jana. Hata hivyo, kutokana na uzoefu wetu wa kushiriki mara kwa mara, tuliweza kupambana na hatimaye kutetea ubingwa wetu," amesema Dismas.

Kwa utani, Dismas amebainisha kuwa kuku wa kienyeji wa Singida ndio siri ya nguvu yao katika ushindi huo.

Kwa upande wake, nahodha wa TANESCO, Mhandisi Ozilias Audax, amesema mchezo ulikuwa mgumu zaidi ya walivyotarajia, lakini wamejivunia kiwango walichoonyesha.

“Hii ni mara yetu ya tatu kushiriki mashindano haya ya Mei Mosi. Wachezaji wetu ni watumishi wa shirika, tunafanya mazoezi kadiri ya ratiba zetu. Mwaka jana tulimaliza nafasi ya tatu, na kadri miaka inavyosonga, mashindano yanakuwa magumu zaidi, hivyo timu zinapaswa kujiandaa kwa nguvu zaidi,” amesema Audax.

Katika mchezo wa kuwania mshindi wa tatu, timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliibuka na ushindi baada ya kuifunga timu ya Dodoma Jiji kwa seti 3-0 (25-5, 25-14 na 25-8).

Aidha, Kamishna wa makocha wa mpira wa wavu mkoa wa Singida, Iddi Nyambi, ameshukuru kwa nafasi ya kuandaa mashindano hayo, akisema imewapa makocha wa mkoa huo fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali za mchezo huo.

Naye mwamuzi wa mchezo huo, Hadija Juma, amesema mashindano ya mwaka huu yamekuwa ya mafanikio makubwa licha ya kupungua kwa idadi ya timu ikilinganishwa na mwaka jana, huku akisisitiza kuwa ushindani umeongezeka

“Ningependa kuona waajiri wakitoa nafasi zaidi kwa watumishi wao kushiriki michezo kama hii, kwani inachangia maendeleo ya afya na mshikamano kazini,” amesema Hadija.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments