TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameelekeza kuundwa kwa timu ya watalaam kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Mbeya kukagua miradi ya maji ambayo imekua sugu katika wilaya ya Rungwe na Busokelo.
Mhe. Aweso (Mb) amesema timu hiyo inatakiwa kuandaa taarifa itakayoonyesha thamani ya miradi hiyo kwasasa na namna ya kuikamilisha kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama ambayo wameisubiri toka mwaka 2009 miradi hiyo ilipoanza.
Mhe. Aweso (Mb) ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya, ambapo katika siku ya tatu amekagua miradi ya maji katika Halmashauri za wilaya za Rungwe, Busokelo na Kyela na kubaini baadhi ya miradi wakandarasi wamejenga miundombinu bila kuwa na uhakika wa chanzo cha maji cha kudumu.
Naibu Waziri Aweso amesema ili kujenga utamaduni wa uwazi na uwajibikaji katika miradi ya maji, wataalam wa maji wanatakiwa kuhakikisha mkandarasi anapolipwa kwa kutekeleza mradi lazima watoe taarifa kwa viongozi ili kujua kiwango cha kazi kilichofanyika. Aidha, amesisitiza watalaam wa maji sio sehemu ya watumishi wa mkandarasi, hivyo malipo ya mkandarasi hayawahusu na hatua zitachukuliwa kwa wale wanaodai malipo kutoka kwa wakandarasi.
Mhe. Aweso (Mb) amesema maji hayana mbadala na kiu ya wananchi ni kupata majisafi na salama, na kuainisha kuwa wakandarasi wanaofanya kazi vizuri kuendana na mkataba malipo ya fedha yatafanyika mara moja.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maji na Umwagiliaji
27.09.2018
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiangalia bomba la maji katika mradi wa maji Kapapa wilayani Busokelo, Mbeya ambapo kisima kinajazwa maji kupima ubora wa kazi ambayo imeshafanyika.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb akipita mashambani kwenda kuangalia vyanzo vya maji wilayani Rungwe.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb ) akisalimiana na baadhi ya wananchi wa kijiji cha kijiji cha Lusanje, kata ya Mpombo –Rungwe mara baada ya kuongea nao katika mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akishuka katika ngazi ya tanki la mradi wa maji Mwakaleli wilayani Rungwe. Mradi huo ni moja kati ya miradi sugu ambayo timu ya wataalam imelekezwa kuipitia na kuandaa taarifa.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb ) akiwa katika eneo la ujenzi wa chujio la maji la mradi wa Kapapa wilayani Busokelo-Mbeya.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akipokea mrejesho kuhusu kero ya majisafi na salama kutoka kwa wananchi wa kata ya Katumba Songwe, wilayani Kyela.
0 Comments