WIZARA YA UJENZI, MAHAKAMA MABINGWA
WAPYA WA KARATA MEI MOSI
Na Mwandishi Wetu, Singida
Wizara ya
Ujenzi na Mahakama wametwaa ubingwa wa mchezo wa karata kwa wanaume na wanawake
katika michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Liti
Mkoani Singida.
Katika
mchezo wa fainali uliokuwa mkali mchezaji Yusufu Nzomoke wa Wizara ya Ujenzi
alimfunga Seif Said wa Wizara ya Uchukuzi kwa magoli 2-1; naye Malkia Nodno wa
Idara ya Mahakama alimfunga Farida Chiwanga wa Ofisi ya Rais Mipango na
Uwekezaji kwa goli 1-0.
Ushindi wa
tatu kwa wanaume umechukuliwa na Magiri Magesa wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini (IRDP); huku ushindi wa tatu kwa wanawake umekwenda kwa Severina
Muyaga wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Bingwa wa
wanaume Yusufu amesema ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki mchezo huo, ulikuwa mgumu katika hatua ya makundi
kutokana na kucheza na wachezaji wazoefu wanaoshiriki kwenye michezo ya
mashirikisho ya Wizara, Idara, Wakala na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) na
Shirikisho la Michezo ya Watumishi wa Umma na Binafsi (SHIMMUTA).
“Ninamshukuru
sana Mungu kwa ushindi huu, pia namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu michezo hii ifanyike,
namshukuru Waziri wangu wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega,” amesema Yusufu.
Naye mshindi
watatu kwa upande wa wanaume, Bw. Magesa amesema michuano ilikuwa ni mizuri
amepambana hadi kufika hatua ya nusu fainali na ameahidi kwenda kujifua zaidi
ili mwakani aweze kutwaa ubingwa.
“Mwaka jana
katika michezo hii pia nilifika hatua ya nusu fainali, lakini mwaka huu
nimeweza kushika nafasi ya tatu, ninaimani nitafanya vizuri zaidi mwakani,
nimeisoma nimeisoma michezo yote ya hatua ya makundi na nitakwenda kufanyia
kazi,” amesema.
Bingwa wa
wanawake, Malkia kutoka Mahakama amesema pamoja na ugeni kwenye michezo hii
ameweza kuwafunga wakongwe hadi kutwaa ubingwa wa mwaka 2025.
Kwa upande
wa mshindi wa tatu kwa wanawake Severina amemshukuru mwajiri wake Ofisi ya
Taifa ya Mashtaka kwa kuthamini michezo.
Naye
msimamizi wa michezo ya jadi kwa mkoa wa Singida, Eliezer Silvester wamesimamia vyema na michezo imeenda kama
ilivyopangwa.
Hatahivyo,
ameiomba serikali kuithamini michezo hii ili iweze kujipambanua zaidi na
kuikuza zaidi.
Wakati huo
huo katika mchezo wa mpira wa kikapu kwa wanaume timu ya Mambo ya Ndani
wametwaa ubingwa kwa kuwafunga Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa pointi
133-58. Ushindi wa tatu umekwenda kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
aliyemshinda Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa pointi 92-58.
Katika
mchezo wa netiboli timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wameingia fainali baada ya
kuwafunga ndugu zao Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora kwa magoli 53-32 mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari
Mwenge.
Nayo Wizara ya
Mambo ya Ndani wameingia fainali sasa kukutana na Ikulu baada ya kuwafunga
Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa kwa magoli 58-53.
Nao mabingwa
watetezi katika mchezo wa mpira wa miguu TANESCO walimetinga kwa kishindo
fainali baada ya kuifunga Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
kwa magoli 4-2.
0 Comments