Naibu waziri wa ofisi ya Waziri mkuu kazi vijana Ajira na watu wenye ulemavu Mhe, Potrobas Katambi
Singida
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Vijana, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, amezitaka
taasisi na wizara zote kuhakikisha kuwa zinatoa ruhusa kwa wafanyakazi wao
kushiriki kikamilifu katika michezo ya Mei Mosi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa michezo ya Mei Mosi
kitaifa, inayofanyika katika uwanja wa CCM LITI mkoani Singida, Mhe. Katambi
amesema michezo si tu burudani bali ni jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano,
mshikamano na afya miongoni mwa watumishi wa umma na sekta binafsi.
"Michezo ni njia ya kujenga afya lakini pia ni sehemu
ya mahusiano bora kazini. Wafanyakazi wakishiriki michezo wanarudi kazini
wakiwa na morali mpya na afya njema," alisema Mhe. Katambi.
Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) taifa, Hery Mkunda alieleza kuwa Mei Mosi ya mwaka
huu itakuwa ya kipekee, si tu kwa ukubwa wa tukio bali kwa namna maandalizi
yalivyofanyika kwa ubunifu na umakini mkubwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Singida,
Dkt. Halima Dendego.
"Mwaka huu Mei Mosi si ya kawaida, Singida imeweka
historia kwa namna ilivyopokea jukumu hili na kulitekeleza kwa weledi.
Tunawashukuru viongozi wa mkoa kwa ushirikiano wao mkubwa," alisema Katibu
huyo wa TUCTA.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mei Mosi
Kitaifa, Bw. Michael Masubo, amepongeza mkoa wa Singida kwa kuonesha utayari
mkubwa na ushirikiano wa karibu katika maandalizi ya michezo hiyo.
“Singida ni mkoa wa kipekee. Nampongeza Mkuu wa Mkoa, Dkt.
Dendego, kwa kushiriki kwa karibu kila hatua ya maandalizi haya na kuhakikisha
kila kitu kinaenda kwa wakati,” alisema Masubo.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Maandalizi ya Mei Mosi, Bw. Alex Temba,
ameongeza kuwa mbali na mashindano ya michezo yanayoendelea, kutakuwa na
matukio mbalimbali ya kijamii na burudani kuelekea kilele cha sherehe hiyo
tarehe 1 Mei.
Akitangaza ratiba ya michezo hiyo, Bw. Temba alieleza kuwa michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, netiboli, kuvuta kamba, na mbio za watumishi itafanyika kwa siku kadhaa kabla ya kilele cha sherehe hiyo ya wafanyakazi duniani.
0 Comments