Singida
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida limeungana na uongozi wa Mkoa huo katika jitihada za ujenzi wa Uwanja wa Bombadia, utakaotumika kwa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Singida.
Sheikh wa
BAKWATA Mkoa wa Singida, Sheikh Issa Nassor, ameongoza msafara wa walimu wa
madrasa (Dini), wanafunzi wa madrasa, pamoja na Katibu wa JUWAKITA Mkoa Bi
Khadija Ommari kwa upande wa wanawake , kwa ajili ya kushiriki kazi za ujenzi
huo kwa vitendo kama ishara ya mshikamano na uzalendo.
Katika ziara yao katika eneo la ujenzi, Sheikh Nassor alipata fursa ya kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, na kueleza namna vijana wa BAKWATA wanavyojitolea kushiriki katika maandalizi ya tukio hilo muhimu. Sheikh Nassor alisema kuwa ushiriki wa taasisi ya dini katika maendeleo ya kijamii ni sehemu ya jukumu la kiimani na kijamii kwa ujumla.
Kwa upande
wake, Mhe. Dendego aliipongeza BAKWATA kwa hatua hiyo ya kizalendo na kuwataka
wadau wengine wa mkoa kuiga mfano huo, akisema kuwa maandalizi ya Mei Mosi ni
suala la kila mwananchi wa Singida kwa kuwa mkoa unakuwa mwenyeji wa tukio la
kitaifa litakalohusisha viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye atakuwa mgeni rasmi.
Naye
Mhandisi Domisianus Kirina kutoka Sekretarieti ya Mkoa – Idara ya Miundombinu,
amesema kuwa hadi sasa ujenzi wa uwanja huo umefikia asilimia 40, huku kazi ya
ukamilishaji wa jukwaa kuu ikiwa inaendelea kwa kasi ili kuhakikisha eneo hilo
linakuwa tayari kwa maadhimisho hayo muhimu.
Uwanja wa
Bombadia unatarajiwa kuwa kitovu cha historia kwa Mkoa wa Singida, si tu kama
mwenyeji wa Mei Mosi 2025, bali pia kama mfano wa ushirikiano wa kijamii kati
ya taasisi za dini, serikali na wananchi kwa ujumla.
0 Comments