Shekh wa mkoa wa Singida Issa bin Nassor akiongea na wanahabari ofisini kwake.
Singida,
Desemba 2, 2024 –
Shekh wa
Mkoa wa Singida, Shekh Issa Nassor, ametoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha
pembejeo za kilimo zinapatikana mapema mkoani Singida kufuatia mvua za masika
ambazo tayari zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Akizungumza
leo katika ofisi yake iliyopo makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) Mkoa wa Singida, Shekh Nassor alieleza kuwa kucheleweshwa kwa
pembejeo kunaweza kusababisha athari kubwa kwa wakulima ambao hutegemea msimu
wa mvua za masika kwa kilimo chao.
“Tunaiomba
serikali na mamlaka husika kuleta pembejeo kwa wakati ili wakulima waweze
kuanza shughuli za kilimo mapema. Huu ni msimu muhimu kwa mkoa wetu ambao
unategemea kwa kiasi kikubwa kilimo cha mvua,” alisema Shekh Nassor.
Aidha, Shekh
Nassor alitoa tahadhari kwa wazazi na waumini wa dini ya Kiislamu kuchukua
hatua za kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo
mafuriko na magonjwa ya mlipuko. Alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa
watoto na familia wakati huu wa mvua.
“Ni jukumu
letu sote, kama waumini na wazazi, kuhakikisha tunalinda familia zetu dhidi ya
athari zinazotokana na mvua hizi. Tujiandae kwa dharura na tuhakikishe mazingira
yetu ni salama,” aliongeza
Shekh Nassor
pia alitoa rai kwa viongozi wa maeneo yenye athari kubwa za mvua kushirikiana
na wananchi katika kutafuta suluhisho la haraka kwa changamoto zinazoweza
kutokea, huku akitoa wito wa mshikamano na maombi katika kipindi hiki.
Taarifa hii
inakuja wakati mvua za masika zikiwa tayari zimeanza kuleta changamoto katika
baadhi ya maeneo mkoani Singida, zikiwemo barabara zisizopitika na mafuriko
yanayohatarisha makazi ya watu.
0 Comments