Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb),akiongea na watumishi katika ukumbi wa bonde mjini Singida.
Eng Lucas Mwinuka meneja Suwasa manyoni akitoa taarifa ya miradi mbalimabli ya maji inayofanyika katika wilaya ya Manyoni.
Singida
Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi
Kundo Andrea Mathew (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Singida (SUWASA) kwa mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji
wake, Sebastian Warioba.
Katika ziara ya kikazi mkoani Singida,
Mhe. Kundo alibainisha kuwa SUWASA imeongeza mapato yake ya kila mwezi kutoka
wastani wa shilingi milioni 290 mwezi Mei 2022 hadi shilingi milioni 380
kufikia Oktoba 2024. Pia, aliipongeza mamlaka hiyo kwa kudhibiti upotevu wa
maji, ambao umepungua kutoka asilimia 33.3 Mei 2022 hadi asilimia 25 kwa sasa.
Mafanikio mengine yaliyotajwa ni
ongezeko la wateja wapya kutoka 15,119 mwezi Mei 2022 hadi 21,211 mwezi Novemba
2024, hatua ambayo inaonyesha juhudi za SUWASA katika kuboresha huduma zake na
kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mhe. Kundo alitoa pongezi hizo baada
ya kupokea taarifa ya hali ya huduma za maji kutoka SUWASA, katika kikao
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bonde la Kati. Kikao hicho kilihusisha
Menejimenti za Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji mkoani Singida,
zikiwemo SUWASA, RUWASA, Bonde la Kati, Maabara ya Ubora wa Maji, Chuo cha
Maji, KIUWASA, na MAUWASA.
Mhe. Kundo alisisitiza kuwa mafanikio
haya ni mfano bora wa usimamizi thabiti na jitihada za pamoja za kuboresha
huduma za maji kwa wananchi wa Singida na Tanzania kwa ujumla.
"Niwapongeze SUWASA kwa kazi
nzuri mnayoendelea kufanya. Mafanikio haya yanaonyesha dhamira ya kweli ya
kuboresha huduma za maji kwa wananchi. Endeleeni na juhudi hizi ili kufikia
malengo makubwa zaidi," alisema Mhe. Kundo.
Mafanikio haya yanaonyesha mchango
mkubwa wa SUWASA katika juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha huduma
za maji safi na usafi wa mazingira nchini.
0 Comments