Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego akiongea na waandishi wa habari katika majumuisho baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika manispaa ya Singida.
Katibu tawala Mkoa wa Singida Dkt Fatma Mganga akiongea katika majumuisho baada ya ziara hiyo.
Na Mwandishi wetu-Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima
Dendego amewaagiza Watendaji katika Halmashauri Saba za mkoa huo kuhakikisha
wanakamilisha utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo hadi kufikia mwisho mwa
mwezi huu.
Mkuu huyo wa mkoa wa Singida ametoa
agizo hilo (14-Aug-2024) katika majumuisho ya ziara yake ya
kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo katika Manispaa ya Singida.
Dendego amesisitiza kuwa miradi
yote iliyoanza kutekelezwa katika kipindi cha miaka Mitatu nyuma lazima
ikamilike ili wananchi waanze kupata huduma mbalimbali za kijamii kwa muda
muafaka.
“Lengo la miradi hii sio kuona
majengo bali ni kutoa huduma inayotakiwa lazima majengo yakamilike kwa wakati
na kwenye matatizo Viongozi wakae na kutatua changamoto hiyo ili miradi
isikwame, Ameeleza Dendego.
Ameeleza kuwa maeneo yote ya miradi
ambayo yana migogoro lazima Viongozi wakae wahusika ili kuondoa changamoto hizo
kwa wakati nia ikiwa ni kuona wananchi waanza kupata huduma bora na za msingi
karibu na maeneo yao.
Dendego pia amepongeza hatua
zinachukuliwa na Watendaji katika kusimamia na kutekeleza miradi hiyo ya
maendeleo ili iweze kutekelezwa kwa Viwango na ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa
mkoa wa Singida Dkt Fatuma Mganga amemhakikishia Mkuu wa wa mkoa wa Singida
kuwa atahakikisha miradi yote inayotekelezwa mkoani humo inakamilika kwa wakati
na kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotolewa.
Dkt Mganga amewasisitiza Watendaji
wote washiriki kikamilifu katika kusimamia miradi iliyopo kwenye maeneo yao ili
wananchi waweze kufurahia huduma bora zinazotolewa na Serikali yao.
Naye, Mkuu wa wilaya ya Singida
Godwin Gondwe ameeleza kuwa atafanya kazi kwa usiku na mchana kwa ushirikiano
na Watendaji wengine ili kuhakikisha miradi yote ya Maendeleo inayotekelezwa
kwenye wilaya yake inakamilika hadi mwisho wa mwezi huu kama maelekezo ya
Serikali yanayotaka.
0 Comments