Na Mwandishi wetu- Singida
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu
imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta mbalimbali katika
kukabiliana na maafa ili kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Singida na
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja
Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua kikao kazi cha
Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji
wa Dhana ya Afya Moja.
Meja Jenerali Mbuge amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la
mwingiliano wa binadamu, wanyama na mazingira ambao husababisha
kutokea kwa magonjwa mbalimbali yanayotoka kwa wanyama na kwenda kwa
binadamu hivyo ipo haja ya kuwepo kwa ushirikiano wa sekta
mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na majanga hayo.
“Tunahuisha mwongozo huu kwa sababu ya mabadiliko ya sheria
na kanuni za usimamizi wa Maafa. Mwongozo huu ni muhimu katika
kurahisisha ushirikiano wa kisekta ili kujenga na kuimarisha ustahimilivu wa
jamii dhidi ya milipuko ya magonjwa na dharura zingine zenye madhara kwa afya
ya binadamu, wanyama na mazingira,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa
husisitiza yakiwemo Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa
(FAO), Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la
Afya ya Wanyama (WOAH) na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa
pamoja husisitiza ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kuwa na mikakati na
sera za pamoja katika kuimarisha afya ya wanadamu, wanyama na mazingira.
“Ili kutekeleza dhana ya Afya moja, ni muhimu kuwa na
miongozo mbalimbali ili kurahishisha uratibu na utendaji katika ngazi zote.
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru FAO ambao walianzisha mchakato wa
kutengeneza mwongozo huu ambao katika kikao hiki utauhuishwa na kutafsiriwa,”
Ameeleza.
Aidha amebainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa ina wajibu wa kuratibu utekelezaji wa dhana ya Afya Moja kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya 2004, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na Mkakati wa Afya Moja 2022-2027.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri
Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza wakati akifungua
kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo
wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.
Baadhi ya Wataalam kutoka sekta mbalimbali wakifuatilia kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.
Mtaalam wa Afya ya Jamii kutoka Shirika la Afya Duniani Bi.
Pelagia Muchuruza akieleza jambo wakati wa kikao hicho.







0 Comments