1. ZAIDI YA WANAWAKE 50 SINGIDA WAPATIWA HATI MILIKI KUPITIA SAMIA ARDHI KLINIKI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Eng Antony Sanga akiongea na kinamama wa Singida katika Samia Ardhi Kliniki inayoendelea sasa.


  Mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida juu ya Samia Ardhi  kliniki inayoendelea sasa mijini hapa

                           

Kamishna Msaidizi wa Adhi Mkoa wa Singida Bi Shamim Hoza akitoa tarifa ya Mkoa


Katibu Mkuu Mhe. Eng Antony Sanga akikabidhi Hati ya Ardhi kwa wanafamia Mke na Mume katika Kliniki Hiyo.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi akitoa hati kwa Mjane aliepimiwa kiwanja katika Kliniki hiyo.


Katibu Mkuu na Mkuu wa Wilaya ya Singida wakisikiliza kero za kinamama na wasichana

SINGIDA:

Zaidi ya wanawake 50 mkoani Singida wamekabidhiwa hati miliki za ardhi kupitia zoezi la Samia Ardhi Kliniki, hatua inayolenga kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi na kuchochea maendeleo yao pamoja na ya familia zao.

Hati hizo zilikabidhiwa Machi 5, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Antony Sanga, katika Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida. Ametoa wito kwa wanawake kujitokeza zaidi kumiliki ardhi kwa kuwa ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema wizara hiyo chini ya Waziri Dkt. Leonard Akwilapo inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi nchini kwa kutoa elimu na kuboresha huduma za sekta ya ardhi.

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la 2023), wanawake na wanaume wana haki sawa ya kumiliki ardhi, hivyo watumishi wa sekta ya ardhi wametakiwa kuhakikisha haki hiyo inatekelezwa bila ubaguzi.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Bi. Shamim Hoza, amesema kupitia Samia Ardhi Kliniki jumla ya wananchi 180 wamehudumiwa, wakiwemo wanawake 144 na wanaume 36. Aidha migogoro 18 ya ardhi imepokelewa ambapo 10 tayari imetatuliwa.

Pia amesema viwanja 18 vimepimwa, zaidi ya shilingi milioni 23 zimekusanywa kama ada za huduma za ardhi, huku zaidi ya wanawake 1,350 wakipatiwa elimu kuhusu haki na taratibu za umiliki wa ardhi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa Halima Dendego, amesema ujio wa Samia Ardhi Kliniki umesaidia kushughulikia changamoto za ardhi kwa wananchi, akibainisha kuwa zaidi ya kesi 900 za ardhi zimeanza kufanyiwa kazi kupitia Kikosi Kazi cha SAMIA.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake walionufaika na huduma hiyo, Bi. Aisha Mohamed ameishukuru serikali kwa kuwaletea kliniki hiyo mkoani Singida akisema imewasaidia wanawake wengi kupima maeneo yao, kupata hati miliki na kuongeza uelewa kuhusu haki za umiliki wa ardhi.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments