Bi Rehema John Mbura mwenyekiti wa shule ya Ilongero akifunga kikao hicho. |
SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la MEDO limeendesha
majadiliano na wadau wa elimu katika Shule ya Msingi Mchanganyiko ya Ilongero
Halmashauri ya wilaya ya Singida kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili
walemavu wa akili.
Akizungumza kwenye majadiliano hayo ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya siku ya walemavu Duniani ambayo hufanyika Disemba 3 kila mwaka,
Mratibu wa shirika hilo Idd Hashim amesema lengo la kukutana na wadau hao ni
kuhakikisha watoto wenye ulemavu wa akili kutokubaguliwa katika Jamii.
Hashim amesema jamii ni lazima itambue walemavu ni watu kama
watu wengine na kwamba ulemavu walionao hawakuhitaji,bali unaweza kumpata mtu
yeyote, hivyo jamii iache kuwaficha watu hao badala yake wawapatie haki zote za
msingi ikiwemo elimu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Sijaona Nkurukwa amesema shule
hiyo imeanzishwa mwaka 1951 huku elimu ya kitengo maalumu ikianzishwa mwaka
2015 ambapo watoto wenye ulemavu wa akili ni 29 wavulana wakiwa 18 wasichana
11.
Diwani wa kata ya Ilongero Mh:Issa Mwiru amewasisitiza
wananchi kulipa kodi ili serikali iendelee kuboresha miundombinu ya shule hasa
kwa upande wa watoto wenye ulemavu wa akili, na kuwaomba viongozi na jamii kwa ujumla
kuwajibika ili kuwaibua wazazi wanaowaficha watoto wao wenye ulemavu huko
majumbani.
Amesema kutokana na shule hiyo kupokea watoto katika maeneo
mengi ya Halmashauri hiyo, hivyo jamii nzima kushirikiana kwa pamoja ili
kuwaboreshea miundombinu ya kujifunzia watoto hao.
Aidha wazazi na wadau kwa ujumla wamesema kuna baadhi ya
wazazi wenye watoto wenye ulemavu huo wanashindwa kuwapeleka watoto wao shuleni
kutokana na shule kutokuwa na mabweni ambapo inamlazima mzazi kumpeleka na
kumrudisha nyumbani mtoto jambo ambalo ni gumu kwao hivyo serikali ingewajengea
watoto hao mabweni.
0 Comments