Matumaini ya Tanzania kufuzu
katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 yataamuliwa kesho
watakaporudiana na Cape Verdea baada ya kukubali kipigo cha goli 3-0 juma
lililopita.
Wakati Tanzania hali ikionekana
kuwa ngumu kwa sasa, nchi jirani za Kenya, Uganda na Burundi hali zao zipo
vizuri na kuna matumaini makubwa kuwa wanaweza kufuzu na kuuwakilisha ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) katika michuano hiyo itakayofanyika nchini
Cameroon.
Tanzania imecheza michezo mitatu
katika Kundi L na kuambulia pointi 2 baada ya kutoka sare mara mbili na
kufungwa mchezo mmoja.
Kocha wa timu ya Tanzania maarufu kama Taifa Stars, Emmanuel
Amunike bado hajakata tamaa, na anawataka Watanzania kuendelea kuwa na imani
kuwa timu yao ina nafasi ya kuelekea Cameroon.
Amunike, ambaye ni nyota wa
zamani wa Nigeria ameliambia gazeti la The Citizen la Tanzania kuwa;
"nafasi bado ipo, kundi letu bado lipo wazi, tunaweza kufanikiwa."
Muelekeo wa safari ya Tanzania
utajulikana kesho Jumanne watakaporudiana na Cape Verde, ni lazima washinde ili
matumaini yao yawe hai. Kama hiyo haitoshi, itawapasa washinde walau mchezo
mmoja na kutoka sare mwengine watakapochuana na Uganda na Lesotho.
Uganda maarufu kama Cranes
wanaongoza Kundi L wakiwa na pointi 7 baada ya kushinda michezo miwili na
kutoka sare mchezo mmoja. Cranes watahitaji alama 4 tu katika michezo mitatu
iliyosalia ili wajihakikishie kufuzu.
Kwa upande wa Kenya, wanaongoza
kundi F wakiwa na pointi 7 baada ya kucheza michezo minne na kushinda miwili,
kupoteza mmoja na kutoka sare mmoja.
Uganda wapo katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa kuongoza kundi L kwa alama saba
Katika michezo miwili iliyosalia
ambapo watacheza na Ghana jijini Accra, na Sierra Leone, Nairobi Harambee Stars
wanahitaji kushinda mchezo mmoja na sare moja ili kufuzu.
Ethiopia ambayo pia inatoka
ukanda wa Cecafa inashika nafasi ya pili katika kundi hilo wakiwa na alama 4
itakuwa na kibarua kizito kugombea nafasi ya kufuzu na Ghana wenye alama 3 na
Sierra Leone wenye alama 2. Yeyote kati ya timu hizo tatu anaweza kuungana na
kinara Kenya kufuzu.
Burundi nao wapo katika nafasi
nzuri ya kufuzu kupitia Kundi C. Mpaka sasa Amavubi wana alama 5 baada ya
kutoka sare michezo miwili na kushinda mmoja. Hatahivyo itawapasa wapigane
vilivyo na Mali wenye pointi 7 na Gabon yenye alama 4 ili kumaliza katika
nafasi mbili za juu na kufuzu.
Kutoka ukanda wa Cecafa tayari mataifa
mawili yapo katika hali mbaya na uwezekano wa kufuzu ni mdogo. Sudani Kusini na
Rwanda hawajaambulia hata alama moja kwenye mechi tatu walizocheza mpaka sasa.
Ili wafuzu, wote, itawapasa washinde
mechi tatu walizosalia nazo, hali ambayo ni ngumu kuyumkinika. Hatahivyo mpira
wa miguu ni mchezo mgumu kutabiri matokeo yake.
0 Comments