Na Jumbe Ismailly MANYONI Sept,12,2018
MKUU wa Wilaya ya Manyoni,Mkoni Singida,Bi Rahabu Mwagisa amepiga marufuku maafisa elimu wa kata wanawake wanaobadili matumizi ya pikipiki walizokabidhiwa kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya elimu na badala yake kuwakabidhi waume zao kwa ajili ya kufanyia shughuli zao binafsi.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa wilaya,Bwana Charles Mkama,Mkuu wa wilaya huyo amesisitiza kwamba kuna baadhi ya maafisa elimu kata wanawake waliojenga utamaduni wa kuwaachia waume zao pikipiki hizo na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.
Aidha Bi Mwagisa amesisitiza kwamba pikipiki hizo hazina budi kutumiwa na maafisa elimu kata wenyewe kwa malengo yaliyokusudiwa na wala siyo vinginevyo na kuonya kwamba vyombo vya usafiri hivyo visitumike kubebea mkaa au kuzitumia kama bodaboda na vitu vingine vinavyoambatana na shughuli hizo.
Awali akimkaribisha kukabidhi pikipiki hizo kwa maafisa elimu wa kata 19 wa wilaya hiyo,Ofisa elimu wa wilaya ya Manyoni,Bwana George Mbesigwe ameweka bayana kwamba mpango huo unaosimamiwa na EQUP Tanzania umeanza kutekelezwa mwaka 2017 na unatarajia kukamilika mwaka 2019.
Ameyataja baadhi ya malengo ya mpango wa Equp Tanzania kuwa ni pamoja na kuimarisha ubora wa matokeo ya kujifunza katika shule za msingi na hasa kwa wasichana,kulenga kuimarisha mfumo wenye gharama nafuu wenye tija ambao unaweza kufanyika kwenye maeneo mengine ya nchi,hususani vijijini.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Bwana Moses Matonya akizungumza katika hafla hiyo amewashauri maafisa elimu wa kata kujenga utamaduni wa kuwasimamia walimu walio chini yao kwa ushiriki mkubwa ili waweze kuleta ufanisi katika mpango huo.
0 Comments