Na Grace Gwamagobe-Afisa Habari Songwe
Ongezeko la hali ya udumavu Mkoani Songwe
inachagizwa na kuwa ni asilimia 25 pekee ya akina mama wote wanaojifungua ndio
huwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa muda wa miezi sita.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Kheri
Kagya ameeleza kuwa udumavu mkoani hapa ni asilimia 37.7 ikiwa na maana kuwa
kati ya watu 100, 37 wanatatizo la udumavu kiwango ambacho ni kikubwa licha ya
Mkoa Songwe kuwa na Vyakula vya kutosha.
“Moja ya sababu kubwa ya ongezeko la udumavu
Mkoani kwetu ni kutokana na akina mama wanaojifungua kutowanyonyesha watoto wao
maziwa pekee kwa kipindi cha miezi sita, hali hii huwafanya watoto kukosa
virutubisho muhimu katika hatua za awali za ukuaji”, amesema Dkt Kagya.
Ameongeza kuwa maziwa ya mama hujenga afya
imara kwa watoto hivyo akina mama wanaojifungua wazingatie ushauri wa wataalamu
wa afya wa kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita, na kisha
kuendelea kunyonyesha na vyakula vingine mbadala mpaka mtoto afikishe umri wa
miaka miwili.
Dkt Kagya amesema maziwa yanayopatikana ndani
ya saa moja baada ya mama kujifungua yana virutubisho vyote kwa
ajili ya ukuaji wa mtoto hivyo akina mama wazingatie hilo huku akiongeza kuwa
ni asilimia 83 ya akina mama wanaojifungua mkoani Songwe huweza kunyonyesha
watoto wao ndani ya saa moja.
“Kumekuwa na visingizio kadhaa kwa akina mama
kutonyonyesha ndani ya saa moja baada ya kujifungua wengine husema maziwa ya
kwanza yenye rangi ya njano kuwa ni machafu, hapana yale maziwa yana
virutubisho vingi vya kwa ajili ya afya njema ya mtoto, pia wengine wanasema
maziwa pekee hayamtoshi mtoto kwakuwa atasaikia kiu, hilo nalo sio sahihi
maziwa ya mama yana kila kitu hata maji pia”, amesisitiza.
Amefafanua kuwa kumekuwa na upotoshaji kuwa
mama mwenye Virusi vya Ukimwi akimnyonyesha mtoto atamuambukiza, kitu ambacho
sio sahihi
Mmoja kati ya akina mama anayeishi na Virusi
vya Ukimwi Grace Kandonga amesema yeye ana watoto wawili ambapo akijifungua
huwa anawanyonyesha maziwa yake pekee kwa miezi sita bila ya kuwapa chakula
kingine na wote hawana maambukizi ya VVU.
Bi Kandonga amesema, “huwa nawanyonyesha
watoto wangu kwa muda wa miezi sita bila kuchanganya na kitu chochote, baada ya
hapo nawapa chakula mbadala kama vile uji na wote wako salama mpaka sasa,
kwahiyo nawashauri akina mama wote tuzingatie ushauri wa wataalamu wa afya na
watoto wetu watakuwa na afya njema”
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt.
Kheri Kagya akitoa zawadi kwa akina mama wa mfano walioweza kunyonyesha watoto
wao maziwa pekee kwa muda wa miezi sita wakati wa maadhimisho ya wiki ya
unyonyeshaji yaliyofanyika Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Akina mama wa mfano walioweza kunyonyesha
watoto wao maziwa pekee kwa muda wa miezi sita wakiwa katika picha ya pamoja na
wadau mbalimbali wanaojishughulisha na afya ya mama na mtoto mkoa wa Songwe.
0 Comments