MANYONI KUKUSANYA JUMLA YA SHILINGI 35,974,965,382/=

HALMASHAURI ya wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida inakadiria kukusanya na kupokea kutoka katika vyanzo mbali mbali vya mapato jumla ya shilingi 35,974,965,382/= katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Akifungua mkutano wa kawaida wa robo ya tatu ya mwaka wa Baraza la Madiwani,Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Bwana Moses Matonya amefafanua kwamba katika kipindi cha mwaka huo wa fedha,Halmashauri hiyo imekusanya na kupokea jumla ya shilingi 17,837,430,083/= ambazo ni sawa na asilimia 50 ya makadirio ya shilingi 35,974,965,382/ kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Aidha Bwana Matonya hata hivyo amesema kwamba Halmashaauri hiyo ilikadiria kutumia jumla ya shilingi 35,974,965,382/= ikiwa ni malipo ya mishahara ya watumishi,matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 na kwamba hadi kufikia mwezi machi,mwaka huu Halmashauri hiyo imetumia shilingi 17,274,080,088/= sawa na asilimia 48 ya makadirio ya shilingi 35,974,965,382/=.


Kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kipindi cha jan hadi machi,Mwenyekiti huyo ameweka wazi kuwa Halmashauri hiyo imekuwa ikitekeleza miradi ya Maendeleo kwenye ngazi ya kata,vijiji na wilaya kwa kutumia fedha za miradi ya maendeleo zilizopokelewa kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Kwa mujibu wa Bwana Matonya katika kipindi cha mwaka wa fedha  wa 2017/2018 jumla ya shilingi 2,639,967,564/=zimepokelewa kati ya shilingi 6,777,772,341/= ikiwa ni sawa na asilimia 38.9 ya fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kisekta ya Programu za miradi ya maji,P4R,Mfuko wa afya (Basket Fund),fedha za mfuko wa jimbo,ukarabati wa Kituo cha Afya Kintinku na shilingi 1,446,506,450/= ni fedha za Mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF).

Hata hivyo Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa madiwani wa Halmashauri hiyo kushirikiana na watendaji wa Halmashauri katika kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vinakusanywa kikamilifu na kutumika ipasavyo.
MWISHO.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments