MBARONI KWA MAHUSIANO YA KIMAPENZI NA WANAFUNZI SINGIDA


VIJANA wanne wakazi wa kijiji cha Misimi  Kata ya  Sepuka wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida Jumapili iliyopita usiku walikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Sepuka wakihusishwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wasichana ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Sepuka.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka kwenye tukio zinasema kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sepuka madukani mzee Selemani Majilanga aliwakuta vijana hao saa 6:00 usiku kwenye nyumba ya Remmi Makhanda wakiwa wamejifungia pamoja na wanafunzi, na inadaiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi hao.
Mwenyekiti Majilanga alitoa taarifa kwa Mkuu wa shule ya sekondari ya Sepuka na alipofika akiwa na wenzake wawili walikwenda kupeleka taarifa Polisi na walipofika wakawakuta na kuwakamata na kuwafikisha kituoni wakawaweka mahabusu na kesho yake siku nzima Polisi walikuwa wakiwahoji kisa cha kuwepo kwenye nyumba hiyo ya wanafunzi usiku.

Vijana hao waliokamatwa na Polisi ni Latifu Abdallah, Abdi Shabani Gunda, Lukuman Alli Satto na Mikidadi Saidi Mteka ambapo wote hawa ni wakazi wa kijiji cha Misimi isipokuwa Lukuman Alli Satto ni wa kijiji cha Mnangana.

Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Sepuka Daudi Hosseah Mkhandi amethibitisha kukamatwa kwa watu hao akiwa na wanafunzi usiku na wamefikishwa tayari Polisi kwa mahojiano na shule iliwapeleka wasichana watano waliokuwa na watu hao usiku kituo cha afya cha Sepuka ili kufanyiwa uchunguzi wa afya zao hata hivyo hawajakutwa na matatizo, na wao waliendelea kuhojiwa na Polisi.

Mwalimu Mkhandi amewataja wasichana hao ambao ni wanafunzi kwenye shule yake kuwa ni Sharifa Mohamed Isumail wa kidato cha kwanza, Sharifa Hassan Ngonyi wa kidato cha pili, Zanura Hassan Dikka wa kidato cha tatu, Fatina Jumanne Mjengi anayesoma kidato cha pili na Lightness Thomas Yaredi anayesoma kidato cha pili.

Uongozi wa shule umesikitishwa sana na tukio hilo la wanafunzi kukutwa usiku wakiwa na kundi la vijana ndani ya nyumba wanazoishi kuashiria kuwepo kwa vitendo vibaya na vinavyokiuka sheria za shule na matokeo yake ni kupoteza masomo na hasara kwa wazazi na taifa.

Uongozi wa shule umewataka wazazi wa wanafunzi kushirikiana na walimu kujua maendeleo ya watoto wao na kubaini mapungufu yaliyopo na kuyakabili mapema ili ufaulu wa masomo kwa  wanafunzi wao uwe mzuri na umetoa onyo kwa pande zote mbili kuacha tabia hiyo mara moja ili wanafunzi wafikie ndoto zao na shule ifikie malengo yake.



Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments