Na,Jumbe Ismailly
IKUNGI
WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imeifunga kwa muda
usiojulikana shule ya msingi ya Taasisi ya madhehebu ya dini ya kiislamu ya
Safina Tunajaa Islamic and English Medium iliyopo tarafa ya Sepuka,wilaya ya
Ikungi,Mkoani Singida kutokana na shule hiyo kutokuwa na usajili kwa zaidi ya
miaka mitatu tangu ilipoanzishwa.
Akithibitisha kufungwa kwa shule hiyo kufuatia ukaguzi
alioufanya siku ya kwanza ya kufungua shule zote,Mratibu wa elimu wa kata ya
Sepuka,mwalimuChitaeli Philipo Kisombo alisema kuwa kwa sababu shule hiyo hiyo
haina usajili,hivyo wanafunzi wangeendelea kukaa bure mpaka darasa la saba.
Hata hivyo Bwana Kisombo amefafanua kwamba wanafunzi waliokuwa
wakisoma darasa la tatu na la nne katika shule hiyo watahamishia katika shule msingi
mama ya Mnang’ana kuanza masomo ya mfumo wa Memkwa na walioandikishwa kuanza
darasa la kwanza wataandikishwa katika shule ya msingi Mnang’ana.
Kwa mujibu wa afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya
elimu wanafunzi hao watarudi na kuendelea na masomo katika shule ya Safina mara
tu baada ya uongozi wa shule hiyo kukakamilisha taratibu za usajili wake,na
wala siyo vinginevyo.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Bwana Idrisa Juma
Mpinji ameweka bayana kwamba pamoja na kwamba siku ya jumatatu ilikuwa ni siku
ya kufungua shule lakini kutokana na barua waliyopokea kutoka wizarani
imewazuia kabisa kufungua shule mpaka hapo maelekezo ya kukamilisha
ujenzi wa vyumba sita vya madarasa,ofisi tatu,stoo,bwalo pamoja na matundu ya
vyoo ya kutosha yatakapokamilishwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnang’ana,Bwana Paskali Juma Mdimi kwa
upande wake amesema kwamba shule hiyo iliyoanzishwa mwak 2015,ilikuwa na jumla
ya walimu wanne na ilifuata taratibu zote za Kijiji,ikiwemo kuomba eneo lenye
ukubwa wa ekari 12 ambazo zilipimwa na kamati ya huduma za jamii.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Safina Tunajaa Islamic and English
Medium Seminary ,Bwana Shabani Saidi Jimbi amebainisha mikakati iliyowekwa na
Kijiji hicho kuwa ni pamoja na kuanzisha michango kwa wazazi wa wanafunzi hao
ili ifakapo mwezi wa tano mwaka huu waweze kukamilisha masharti yaliyowekwa na
wizara hiyo.
MWISHO.
0 Comments