Bao pekee lililofungwa dakika ya 70 na Mzambia Obrey
Chirwa, limeirudisha kileleni mwa msimamo wa ligi yaVodacom na kurudisha
matumaini ya mabingwa hao watetezi kutetea taji lao msimu huu.
Yanga iliyocheza bila nyota wake watano wa kikosi cha kwanza,
ililazimika kupambana kiume hadi kupata bao hilo ambalo lilitokana na uzembe wa
beki Yakubu Mohamed na kipa Aishi Manula.
Ushindi wa leo unaifanya Yanga kufikisha pointi 56, katika
michezo 25 waliyocheza na kuiacha Simba nafasi ya pili wakiwa na pointi 55,
huku kesho timu hiyo ikiwa na kibarua kigumu dhidi ya Kagera Sugar.
Katika mchezo wa leo Yanga ilijikuta ikiongeza idadi ya majeruhi
kwenye kikosi chake baada ya kiungo Justine Zullu, kuvunjika mguu dakika ya 27
baada ya kuchomekewa mguu na nahodha wa Azam Himid Mao, wakati akijaribu
kufunga baada ya pasi nzuri kutoka kwa Simon Msuva.
Azam waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi leo
waliuanza mchezo huo kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la
Yanga lakini mshambuliaji wa Ghana Yahya Mohamed na Ramadhani Singano
walishindwa kuzitumia nafasi walizozipata.
Yanga walionekana kujipanga vizuri dakika ya 27 baada ya Zullu
kupata nafasi hiyo na kupiga juu huku akiumizwa mguu na kutolewa nje na nafasi
yake kuchukuliwa na Emmanuel Maritini aliyekwenda kusaidiana na Haruna
Niyonzima na Chirwa.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa bado hazijafungana na Azam
walionekana kuutawala mchezo na kuwazidi Yanga ambao walionekana kuzidiwa kila
idara.
Kiungo Salum Abubakar angeweza kuifungia timu yake ya Azam bao
la kuongoza dakika ya 43, baada ya kuuwahi mpira ambao Vicent Bossou, alikuwa
akimrudishia kipa Deogratius Munishi lakini kipa huyo alifanya kazi ya ziada
kwa kuokoa mpira huo.
Kipindi cha pili Yanga walikianza kwa kasi baada ya kufanya
mashambulizi mawili ya nguvu kwenye lango la Azam lakini Msuva na Chirwa
walizipoteza nafasi hizo.
Katika dakika ya 63 mshambuliaji wa Azam Samweli Afful, aliyeingia
kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Yahya Mohamed alipoteza nafasi ya wazi
baada ya shuti alilopiga kwenda nje akiwa amebaki na kipa wa Yanga Dida.
Dakika ya 70, Chirwa aliwainua vitini mashabiki wa timu yake
baada ya makosa ya wachezaji wa Azam kutegeana mpira uliokuwa anarudishiwa kipa
Munishi na mfungaji aliuwahi na kumpiga chenga beki Yakubu Mohamed na kupiga
shuti ambalo liligonga mwamba wa juu na kutinga wavuni.
Bao hilo lilionekana kuwazindua Azam ambao waliongeza kasi ya
mchezo kwa kulishambulia lango la Yanga lakini presha yao ilikuwa ikiishia
miguuni mwa mabeki wa Yanga Bossou na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Katika mchezo Azam FC, waibadilisha wachezaji watatu ambapo
walimtoa Mohamed na kuingiza Afful, Ramadhani Singano aliingia Broce Kagwa na
Shabani Idd nafasi yake ikachukuliwa na Joseph Mahundi.
Kwa uapande wa Yanga alitoka Zulu baada ya kuumia akaingia
Martin, Deusi Kaseke nafasi yake ikachukuliwa na Geofrey Mwashiuya na dakika za
mwisho alitoka Msuva na nafasi yake kuingia Juma Mahadhi.
Huo ni ushindi wa kwanza mbele ya Azam kwa kocha George
Lwandamina ambaye ameichukua timu hiyo mwanzoni mwa mzunguko wa pili akimrithi
Mdachi Hans van der Pluijm.
0 Comments