Diwani wa kata ya Unyanga Geofrey Mdama akizungumza na wananchi katika mkutano huo. |
WIMBI
la kuwaondoa viongozi wa serikali za vijiji limezidi kupamba moto Mkoani
Singida ambapo katika Kijiji cha Unyianga,Manispaa ya Singida mkutano mkuu wa
Kijiji hicho umemvua madaraka Mwenyekiti wa Kijiji,Bwana Sombi Omari Goda
pamoja na wajumbe wa serikali ya Kijiji hicho kutokana na tuhuma za kushindwa
kusoma taarifa ya mapato na matumizi ya Kijiji hicho kwa kipindi cha miaka
mitatu.
Aidha
wananchi hao walioonekana wakiwa na tayari na maamuzi ya tuhuma kabla ya
mkutano huo huku wakiwa na hasira kwa viongozi wao hao wamezitaja tuhuma
zingine za kuwaondoa madarakani wawakilishi wao hao kuwa ni kushindwa kusimamia
mapato na matumizi ya fedha za Kijiji hicho.
Maamuzi
hayo yamefikiwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Kijiji cha Unyianga uliofanyika
kwenye viwanja vya mikutano vya ofisi za Kijiji hicho na kupiga kura za
kumkataa mwenyekiri wa Kijiji pamoja na wajumbe wote wa serikali ya Kijiji
hicho na kuwataka wakae pembeni kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Katika
mkutano huo uliohudhuriwa na zaidi ya watu mia tatu,akiwemo diwani wa kata ya
Unyianga,Bwana Geofrey Mdama nusura uvunjike baada ya Mwenyekiti wa Kijiji
hicho na baadhi ya wajumbe wa serikali ya Kijiji kuwashauri wananchi hao kwamba
kwa kuwa mtendaji aliyepaswa kusoma taarifa ya mapato na matumizi hakuwa
tayari kusoma taarifa hiyo,hivyo hawana budi kusamehe yote yaliyojitokeza na
kuanza kukijenga upya Kijiji chao.
Hata
hivyo wananchi hao bila kujali itikadi za vyama vyao na wala jinsia zao kwa
pamoja waliamua kuanza kupiga kelele na kususia kuendelea kuwepo kwenye uwanja
wa mkutano huo na kuondoka na kuwaacha viongozi wakiwa wamekaa kwenye meza
ambapo baada ya kushauriwa na ofisa mtendaji wao ndipo walipoamua kurudi
kuendelea na mkutano huo.
Kwa
upande wake Ofisa Mtendaji wa kata ya Unyianga,Bi Habiba Juma amewahakikisha
wananchi hao kwamba walichokuwa wakidai ni haki yao kabisa ya kusomewa taarifa
ya mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu na kwamba kuanzia mwezi wa
kumi hadi sasa hakuna mapato yeyote yaliyokusanywa kwenye vibanda vilivyopo
Kijijini humo.
Naye
diwani wa kata ya Unyianga,Bwana Geofrey Mdama ameweka bayana kuwa baada ya
wananchi walioanza kususia mkutano huo kurejea tena kwenye viwanja
hivyo,ametumia fursa hiyo kuwataka watoe maamuzi wanayodhani yataleta tija kwa
upande wao na Kijiji hicho kwa ujumla na ndipo walipopendekeza kura ipigwe
kupata muafaka wa suala hilo.
0 Comments