Waziri Anthony Mavunde akiongea na wanachi wa kijiji cha Nyasa ,Kata ya Kang"ata Wilaya ya Handeni
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni Mhe. Amiri Changogo akizungumza mbele ya waziri wa Madini Anthon Mavunde.
SINGIDA
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony
Mavunde, ameeleza kuwa Mgodi wa Kati wa Dhahabu wa Magambazi uliopo Wilayani
Handeni Mkoani Tanga utaanza kufanya kazi rasmi ifikapo Julai 2025 na
unatarajiwa kuleta tija kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika
Kijiji cha Nyasa na Wilaya ya Handeni kwa ujumla.
Waziri Mavunde ameeleza hayo leo Mei
10, 2025, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Kijiji cha Nyasa, Kata ya Kang’ata, Wilaya ya Handeni, ambapo amekuja kuleta
mrejesho wa ahadi aliyotoa Aprili 6, 2025 kuhusu hatma ya uendelezaji wa mgodi
huo uliosubiriwa kwa muda mrefu.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kuhakikisha Mgodi huu wa Magambazi
unaanza kufanya kazi na kuwainua wananchi wa hapa na mnyororo mzima wa shughuli
za maendeleo.
Baada ya kuchukua hatua ya kupata
muafaka wa kuhakikisha mgodi huo unaanza kufanya kazi, Kampuni nyingine ya tatu
itateuliwa ndani ya siku 14 kuanzia Mei 12 hadi Mei 26, ambayo itaungana na
Kampuni za PMM na East African Metals/CANACO ili kuendesha mgodi huo.
Kipekee nawashukuru sana wananchi wa
Nyasa kwa uvumilivu wenu, hili jambo lilikuwa la muda mrefu tangu tumeanza
kulifanyia kazi, mlikubali kukaa hapa na kunyeshewa na mvua, na leo mmekuja
tena na kukubali kukaa nami kwenye mvua ili kuwapa mrejesho wenu.
Kampuni zinazoendesha mgodi huo
kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa wakazi wa Nyasa katika ajira ili wananchi wa
Nyasa wanufaike moja kwa moja na uwepo wa mgodi huo katika Kijiji chao.
Faida zitakazopatikana ikiwa ni pamoja
na kuinua mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, uboreshaji wa miundombinu
ya afya, elimu, barabara na mengine kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR)
pamoja na ushiriki wa Watanzania katika mgodi huo kwa kutoa huduma na kuuza
bidhaa (Local Content)”amesema Mavunde
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Mhe. Amiri Changogo, Mkuu wa Wilaya ya
Handeni, Mhe. Japhari Kubecha, na Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhe. John Sallu,
wamemshukuru Waziri Mavunde kwa kufanyia kazi suala hilo na hatimaye kuondoa
kiu ya muda mrefu ya wananchi wa Nyasa na Handeni kwa ujumla.
Naye, Wakili Albert Msando (aliyekuwa
Mkuu wa Wilaya Handeni, hivi sasa ni Mkuu wa Wilaya Ubungo) ameeleza hisia zake
za kufurahishwa na hatua hiyo kwani alikuwa akilisimamia kwa ukaribu kipindi
akiwa Mkuu wa Wilaya hiyo na kwamba hana deni na wananchi wa Kata ya Kang’ata
na Kijiji cha Nyasa baada ya kutatuliwa kwa changamoto hiyo iliyokuwa
inawakabili kwa muda mrefu.
0 Comments