Katibu tawal mkoa wa Singida Dkt Fatuma Mganga akifunga kambi ya madakitari bingwa bobezi wa Dkt Samia baada ya kutoa huduma kwa Siku tano mkoani Singida.
SINGIDA
Wananchi wa
mkoa wa Singida wameonyesha shukrani na furaha yao kwa Serikali baada ya kupata
huduma bora za afya kupitia kambi ya madaktari bingwa bobezi wa Dkt Samia. Wamesema huduma
hizo zimekuwa mkombozi mkubwa, hasa kwa wale wanaoishi vijijini na ambao mara
nyingi hukosa huduma za kibingwa kwa ukaribu.
Kwa muda wa siku tano, madaktari bingwa wamekuwa wakitoa huduma bure kwa maelfu ya wananchi wa Singida katika maeneo mbalimbali ya afya.
Baadhi ya wananchi waliohudumiwa wamesema kuwa wameguswa na moyo wa huruma na umahiri ulioonyeshwa na madaktari hao. Wameeleza kuwa wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kibingwa, lakini kupitia kambi hii, walizipata karibu na makazi yao.
“Huduma hizi
ni msaada mkubwa sana kwetu. Tunaomba Serikali iendelee kuleta madaktari hawa
mara kwa mara.”
Mwenyekiti
wa madaktari bingwa bobezi wa Samia, Dkt. Amani Malima, amesema kuwa katika siku tano
pekee, jumla ya wagonjwa 3,242 walipatiwa huduma mbalimbali, huku wagonjwa 82
wakifanyiwa upasuaji.
“Tumefanikisha
matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo upasuaji, macho, masikio, mifupa na
mengineyo. Tunafurahi kuona kuwa tumewafikia wananchi wengi,” amesema Dkt.
Malima.
Akifunga
rasmi kambi hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, alitoa
pongezi kwa timu ya madaktari bingwa kwa kazi nzuri waliyoifanya.
“Tunawakaribisha
tena mara nyingine. Singida bado inawahitaji. Hii ni hatua kubwa katika
kuimarisha sekta ya afya mkoani kwetu,” alisema Dkt. Fatuma.
Kambi ya
madaktari bingwa wa Samia mkoani Singida ni sehemu ya awamu ya tatu kwa Kanda
ya Kati, baada ya huduma kama hizo kutolewa katika mikoa ya Morogoro na Iringa.
Lengo kuu la mpango huu ni kufikisha huduma za kibingwa karibu na wananchi
wote, hasa walioko maeneo ya mbali.
0 Comments