GULAMALI ACHANGIA MILIONI 38 UJENZI WA OFISI ZA CCM MKOA WA SINGIDA.





 Mwandishi Wetu, SINGIDA

MWEKA Hazina mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Haidary Gulamali, ameahidi kuchangia shilingi milioni 19 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la ofisi za CCM Mkoa wa Singida.Huku akichangia milioni 20 kwaajili ya jumuiya ya Umoja wa Vijana UVCCM.Mkoa wa Singida.

Gulamali ambaye aliwahi kugombea ubunge kupitia CCM awamu mbili katika jimbo la Singida Kaskazini, alitoa ahadi hiyo jana wakati wa hafla ya chakula cha jioni ilichoandaliwa na viongozi wa CCM mkoa wa Singida kwa ajili ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi.

Gulamali alisema anatoa mchango huo ili jengo hilo ambalo limekaa muda mrefu bila kumalizika ujenzi wake uweze kumalizika haraka na shughuli mbalimbali za chama ziweze kuendelea.

Gulamali ambaye kwa sasa ni mwanachama alisema anapenda kukiunga mkono chama chake cha CCM ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Katika hafla hiyo jumla Sh.milioni 200 zilichangwa na viongozi mbalimbali walioshiriki ambapo katika kuhakikisha ujenzi wa ofisi hizo unakamilika kwa haraka kuliundwa kamati itakayosimamia ujenzi.

Aidha, Gulamali mbali na kushiriki hafla hiyo ya kuchangia fedha za kumalizia ujenzi wa ofisi za CCM, pia alishiriki ziara ya Katibu Mkuu wa CCM jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Bombadia mjini Singida na pia wakati wa kumuaga Dk.Nchimbi katika kijiji cha Itaja jimbo la Singida Kaskazini.

Dk.Nchimbi na msafara wake wameanza ziara leo katika Mkoa wa Manyara baada ya kuhitimisha katika mkoa wa Singida ambao alianza Mei 29, 2024.


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments