MKALAMA YAWEKA KIPAUMBELE ELIMU, AFYA NA MIUNDOMBINU MWAKA WA FEDHA 2026/27

  


Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mkalama Hajjat Asia Messos akitoa taarifa ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya Halmshari ya Wilaya ya Mkalama kwa wanahabari.


Na Cales Katemana

Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imesema itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/27, ikilenga kuboresha huduma za elimu, afya pamoja na miundombinu ya utawala kwa manufaa ya wananchi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat  Asia Messos  wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wilaya kwa waandishi wa habari wilayani Mkalama.

Hajjat Asia amesema katika sekta ya elimu, halmashauri itajenga Shule mpya ya Sekondari Ishenga kupitia mradi wa SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 544, sambamba na kukamilisha maabara katika shule za sekondari za Isanzu na Mwangeza, madarasa katika shule za msingi za Ndala, Migunga na Mgolombyo, pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za Malaja, Ilunda na Kinandili.

Aidha, amesema kutakamilishwa nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Kipamba, kujengwa bweni katika Shule ya Sekondari Gunda, kutengenezwa vitanda 40 katika Shule ya Sekondari Mwangeza pamoja na kununuliwa vifaa vya TEHAMA kwa Shule ya Sekondari Nduguti.

Katika sekta ya utawala, amesema halmashauri itajenga nyumba tatu za wakuu wa idara kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi, huku katika sekta ya afya ikikamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vya Ilunda na Gumanga.

Mkurugenzi huyo amesema pia halmashauri itaendelea kuweka msisitizo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuboresha huduma za elimu, afya, kilimo na mifugo ili kuongeza ustawi wa wananchi na kuharakisha maendeleo ya wilaya.

Akizungumzia mafanikio ya mwaka wa fedha 2025/26, Hajjat Asia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais kwa kuendelea kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, hatua ambayo amesema imechangia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Pia amewapongeza watumishi wa halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mohamed Juma, Baraza la Madiwani pamoja na wananchi wa Mkalama kwa ushirikiano wao katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hajjat Asia amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu au uvunjifu wa amani kwa viongozi wa vijiji na kata au Ofisi ya Mkurugenzi.

Kwa upande wa watumishi wa umma, amewahimiza kuongeza uwajibikaji, ubunifu na kasi ya utendaji kazi ili kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza kuwa maendeleo ya Wilaya ya Mkalama yanategemea mshikamano na ushirikiano wa kila mmoja.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments