Singida | 04.04.2025
Maandalizi ya
sherehe za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yamepamba moto mkoani Singida! Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ameongoza ziara maalum katika eneo
maarufu la Ubungo, linalotambulika kwa biashara ya nyama ya kuku wa kienyeji,
hususan wakati wa usiku.
Ziara hiyo
ilikuwa na lengo la kujionea jinsi huduma zinavyoendelea, hasa kwa kuzingatia
kuwa mkoa huu utaandaa sherehe za Mei Mosi kwa ngazi ya taifa. Akiwa ameambatana
na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe,
Meya wa Manispaa ya Singida, Mhe. Yagi Kiarau, pamoja na viongozi wa CCM mkoa
na wilaya, walipata fursa ya kuzungumza na wafanyabiashara wa kuku wa kienyeji
kuhusu maandalizi yao kwa ajili ya kupokea wageni.
Katika mazungumzo na Katibu wa Wachoma Kuku Ubungo, Almasi Mkoko, imebainika
kuwa wafanyabiashara hao wamejipanga vyema kuhakikisha wageni wanaofika Singida
kwa sherehe za Mei Mosi wanapata huduma bora.
Mkuu wa Mkoa,
Mhe. Halima Dendego, amesema kuwa zaidi ya wageni elfu sita wanatarajiwa
kuhudhuria sherehe hizo, na hivyo ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa chakula
na malazi kuhakikisha huduma zao zinakuwa za viwango vya juu.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Mhe. Yagi Kiarau, amethibitisha kuwa
Manispaa imejipanga kuhakikisha usalama katika maeneo yote ya wageni, ikiwa ni
pamoja na eneo la Ubungo.
0 Comments