Singida
Katika kuadhimisha kumbukizi ya siku
ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
kongamano maalum limepangwa kufanyika tarehe 13 Aprili 2025 jijini Dodoma.
Tukio hilo litahusisha mijadala ya kitaifa, maonyesho mbalimbali, na shughuli
za kihistoria zitakazomulika mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere katika harakati
za uhuru, ujenzi wa mshikamano wa kitaifa, na maendeleo ya Tanzania.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.
Kauli hiyo ilitolewa katika kikao cha
kwanza cha uongozi mpya wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Wilaya ya Singida,
kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Walimu Nyerere, mjini Singida.
Akizungumza katika kikao hicho,
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Singida, Rajab Shabani Musa,
alitoa wito kwa viongozi wa ngazi zote kuiga na kuyaishi kwa vitendo maadili
mema na misingi bora ya uongozi aliyoiacha Baba wa Taifa.
"Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi
mwenye maono makubwa, mzalendo wa kweli na mpenda haki. Ni jukumu letu kama
viongozi na wananchi kuyatunza maadili yake na kuyatumia kama dira ya maendeleo,"
alisema Rajab Musa.
Katika kudumisha maadili na historia
hiyo kwa vizazi vijavyo, Mkoa wa Singida umeamua kuunda tume maalum chini ya
mlezi wa taasisi hiyo mkoani, Mheshimiwa Halima Dendego. Tume hiyo itakuwa na
jukumu la kutembelea, kutambua na kuhifadhi maeneo yote aliyowahi kufika Baba
wa Taifa wakati wa uhai wake ndani ya Mkoa wa Singida.
Hatua hiyo inalenga kuyaweka maeneo
hayo kama urithi wa taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo, sambamba na kuimarisha
kumbukumbu ya mchango wa Mwalimu Nyerere katika maendeleo ya Mkoa wa Singida na
Tanzania kwa ujumla.
Aidha, taasisi hiyo imetoa wito kwa
wananchi wote, hususan vijana, kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali
za kumbukizi hizo, kwa lengo la kujifunza, kuhifadhi historia na kuendeleza
mazuri yote aliyoyaacha Baba wa Taifa.
0 Comments