Katibu wa Bakwata Mkoa Singida Omari Ally Muna akiongea katika Iftari hiyo.

Singida
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassor, ameziomba mamlaka husika pamoja na taasisi za kumbukumbu ya historia ya machifu nchini kuhakikisha zinafanya mpango wa kuleta kumbukumbu za Malkia Liti nchini. Amesema hatua hiyo itakuwa muhimu katika kuhifadhi historia ya Mkoa wa Singida na kuzihifadhi kumbukumbu hizo katika makumbusho ya mkoa huo.
Sheikh Nassor aliyasema hayo katika futari maalum iliyoandaliwa na familia ya Jafari Saidi Mtoro kwa kushirikiana na kamati maalum ya Ofisi ya BAKWATA Mkoa wa Singida. Alieleza kuwa amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali kuhusu mabaki ya Malkia Liti kutorejeshwa nchini, hasa mkoani Singida, kama ilivyofanyika kwa machifu wengine kama Chief Mkwawa.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kuwa na jengo maalum la kumbukumbu ya historia ya Mkoa wa Singida, ili kuhifadhi na kuonesha tamaduni, asili, mila, na desturi za mababu zetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Jafari Saidi Mtoro, akitoa neno la shukrani kwa wageni waliohudhuria iftar hiyo, ameushukuru uongozi wa BAKWATA Mkoa wa Singida na wote walioshiriki. Aidha, ametoa wito kwa wakazi wa Singida kuchangamkia fursa ya maadhimisho ya Mei Mosi yatakayofanyika kitaifa mkoani humo, akisisitiza kuwa ni nafasi muhimu kwa wananchi wa Singida kuonesha ukarimu kwa wageni watakaofika.
0 Comments