Singida,
12 Machi 2025
Jeshi la Polisi mkoani Singida
limeendelea na juhudi zake za kudhibiti uhalifu baada ya kuwakamata jumla ya
watuhumiwa 28 kwa makosa mbalimbali ya jinai. Hatua hii ni sehemu ya mpango wa
kuhakikisha usalama na utulivu kwa wakazi wa mkoa huu.
Akizungumza na waandishi wa habari
katika makao makuu ya jeshi hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, SACP Aemon
Kakwale, amesema kuwa jeshi lake limefanikiwa kusimamia sheria kwa ufanisi,
ikiwa ni pamoja na operesheni kali dhidi ya makosa ya usalama barabarani.
Katika mwezi wa Februari pekee, makosa ya usalama barabarani 3,580 yalibainika, ambapo 3,577 yalihusisha madereva waliotozwa faini na kuruhusiwa kuendelea na safari baada ya kufuata taratibu za kisheria.
Kwa upande wa mafanikio ya kesi
mahakamani, Kamanda Kakwale amesema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kufikisha
jumla ya kesi 30 mahakamani, ambapo wahusika walihukumiwa vifungo kulingana na
makosa yao.
Katika hukumu hizo, mtuhumiwa mmoja
amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kosa la kujaribu kubaka, huku kesi
nyingine zikiendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida
linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na
usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kusaidia kudumisha amani na utulivu
katika jamii.
0 Comments