Na Happiness Shayo – Arusha
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Utalii imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ya ujenzi wa barabara (km 30) kwa
gharama za shilingi milioni 256 pamoja na ujenzi wa bwawa kwa gharama ya shilingi
milioni 125 katika Hifadhi ya Wanyamapori Makuyuni iliyopo Wilayani Monduli
Mkoani Arusha ikiwa ni mojawapo ya maboresho katika kuendeleza uhifadhi, kukuza
utalii na uwekezaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe.Timotheo Mnzava ameyasema hayo leo
Machi 13,2025 wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua miradi hiyo Mkoani
Arusha.
"Kipekee tuwapongeze TAWA
wanafanya kazi nzuri hasa katika
kazi ya ukarabati na ufunguaji wa
barabara na kazi ya utengenezaji wa bwawa" amesisitiza Mhe.Mnzava.
Aidha, Mhe. Mnzava ametoa wito kwa
Menejimenti ya TAWA kuendelea kuitangaza hifadhi hiyo ili malengo
yaliyokusudiwa, kutatua migogoro ya mipaka na kujenga mahusiano mazuri na jamii
inayozunguka hifadhi hiyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Mnzava
amesema matamanio ya kamati hiyo ni kuiona TAWA inaendelea kubuni na kuwaza
vyanzo vingine vya mapato ili iweze kujiendesha bila kutegemea fedha kutoka
Serikali kuu.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Balozi, Dkt.Pindi Chana (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa maelekezo inayoyatoa mara kwa mara kwa
Wizara yake ambapo amesisitiza kupitia maekezo hayo Wizara ya Maliasili na Utalii imeweza
kutekeleza na kuisimamia vizuri TAWA.
" Tunashukuru kwa maelekezo ya
kamati lakini napenda kuielekeza TAWA hakikisheni hakuna migogoro ya mipaka na
wakati umefika wa kulinda misitu yetu kwa sayansi na teknolojia mfano kwq
kutumia kamera za kisasa, drones ili kuepusha uvamizi na ujangili" Mhe.
Chana amesisitiza.
Pia, Mhe. Chana ametia mkazo suala la
TAWA kujitangaza huku akiitaka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuhakikisha
hifadhi hiyo inatangazwa ipasavyo ili kuvutia watalii.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu,
Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia Maliasili) CP Benedict
Wakulyamba amesema kuwa Wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana
na wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuchimba mabwawa, uongezaji wa vituo
vya askari na kutumia teknolojia mbalimbali.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Utalii iko Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi.
0 Comments