Waziri wa Madini Antony Mavunde akiongea na wadau wa madini Mororogoro.
Rais wa Shirikisho la wachimbaji Madini Nchini Femata John Wambura Bina akiongea katika kikao kazi hicho.
Morogoro, Tanzania
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony
Mavunde, amepiga marufuku wageni kuingia na kufanya shughuli za uchimbaji wa
madini kwenye leseni za wachimbaji wadogo bila kufuata taratibu za kisheria.
Hatua hii inakuja baada ya kugundulika changamoto katika mikataba ya utoaji wa
msaada wa kiufundi kati ya wamiliki wa leseni ndogo za uchimbaji na wageni.
Mavunde alitoa tamko hilo leo,
Februari 17, 2025, wakati wa kufungua Kikao Kazi cha wadau wa madini
kilicholenga kupokea maoni juu ya rasimu ya Kanuni za Madini za Utoaji Msaada
wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji wa Madini. Mkutano huo
umefanyika katika Ukumbi wa Edema Hoteli, Morogoro.
Akihimiza ushiriki wa wadau, Waziri Mavunde alisisitiza umuhimu wa kupata maoni ya wazi na yenye tija kwa ajili ya kuandaa kanuni bora zinazotekelezeka ili kuboresha sekta ya madini nchini. Pia alibainisha kuwa mabadiliko makubwa katika sekta hiyo yanatokana na utashi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anahimiza maendeleo kwa wachimbaji wadogo.
"Haiwezekani mgeni aje, apate
nafasi kupitia mkataba wa utoaji msaada wa kiufundi, lakini wachimbaji wadogo
hawapati manufaa wala uboreshaji wa teknolojia na mitaji. Hili halikuwa lengo
la sheria," alisema Mavunde.
Aidha, Waziri ametoa onyo kali kwa
wachimbaji wadogo wanaowaruhusu wageni kuingia kinyemela kwenye leseni zao,
akisema kuwa hatua kali, ikiwemo kufutiwa leseni, zitachukuliwa kwa
watakaokiuka agizo hilo. Vilevile, amewaagiza Maafisa Madini wa Kanda (RMO)
kuhakikisha wanadhibiti uingiaji wa wageni kwenye leseni ndogo bila kufuata taratibu
husika.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema kikao hicho kinalenga kupata maoni ya
wadau ili kuandaa rasimu ya kanuni hizo kwa uwazi na ushirikishwaji wa pande
zote.
Naye Rais wa Shirikisho la Wachimbaji
Wadogo wa Madini Tanzania, John Bina, amepongeza hatua ya serikali ya
kuwashirikisha wadau katika uandaaji wa kanuni hizo, akisema kuwa
ushirikishwaji huo utahakikisha kanuni zinazoandaliwa zinazingatia mahitaji
halisi ya wachimbaji wadogo.
Mkutano huo umehudhuriwa na wadau
mbalimbali wa sekta ya madini, wakiwemo viongozi wa wachimbaji wadogo kutoka
mikoa yote nchini, vyama vya wachimbaji wadogo wanawake, na wafanyabiashara wa
madini.
0 Comments