Na Mwandishi wetu
Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya
Cuba zimekubaliana kushirikiana katika sekta ya utalii na uhifadhi wa
wanyamapori, hasa katika kukabiliana na changamoto ya mimea vamizi ndani ya
maeneo yaliyohifadhiwa.
Makubaliano haya yamefikiwa , Februari
16 , 2025, katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Ujumbe wa Cuba
umeongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole, pamoja na
Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera, huku upande wa
Tanzania ukiwakilishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt.
Pindi Chana (Mb).
Waziri Dkt. Pindi Chana amewakaribisha
nchini wataalamu saba kutoka Cuba kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina kuhusu
mimea vamizi inayozikumba hifadhi za taifa. Utafiti huu unalenga kutafuta
suluhisho madhubuti katika kuimarisha uhifadhi wa maliasili.
"Mimea vamizi ni tishio kubwa kwa
uhifadhi nchini, hasa katika Hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro na Bonde la Ziwa
Victoria. Spishi hizi zimevuruga mifumo ya ikolojia, kuathiri makazi ya wanyamapori,
utalii, na maisha ya jamii za wenyeji," amesema Mhe. Chana.
Ameeleza kuwa mimea vamizi imeenea
kutokana na shughuli za kibinadamu kama kilimo, biashara ya mimea ya mapambo,
na juhudi za kudhibiti mmomonyoko wa ardhi. Kupitia ushirikiano huu, Tanzania
itanufaika na teknolojia ya kisasa kutoka Cuba ili kukabiliana na changamoto
hii na kuimarisha uhifadhi wa maliasili.
#Tanzania #Cuba #Uhifadhi #Utalii
#MimeaVamizi #Serengeti #Ngorongoro
0 Comments