Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa, na Michezo, Hamis Mwinjuma, amewataka waandishi wa habari kuhakikisha
wanatoa taarifa sahihi na zisizoegemea upande wowote kuhusu Uchaguzi Mkuu wa
2025 utakaohusisha uchaguzi wa Madiwani, Wabunge, na Rais.
Akizungumza leo, Februari 14, 2025,
jijini Dodoma wakati wa kufunga mkutano wa mwaka wa vyombo vya utangazaji
ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mwinjuma amesema
mafunzo yaliyotolewa yamewawezesha waandishi kuboresha taaluma yao, hasa katika
utoaji wa taarifa sahihi kuelekea uchaguzi huo.
"Vyombo vya habari vina nafasi
muhimu katika uchaguzi huu. Taarifa zisizo sahihi zinaweza kudhoofisha
demokrasia, hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha umma unapata habari za kweli ili
kufanya maamuzi sahihi," amesema Mwinjuma.
Amehimiza pia matumizi sahihi ya
Kiswahili katika utangazaji ili kulinda na kuendeleza lugha hiyo, akisisitiza
kuwa ni muhimu kuitumia kwa ufasaha.
Aidha, amebainisha kuwa serikali inaendelea kushirikiana na sekta ya habari, huku akisisitiza kuwa Wizara yake iko wazi kwa mawasiliano. Pia, amekumbusha kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuikuza sekta hiyo, jambo lililoonekana kupitia hatua yake ya kufungua vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, amewataka waandishi wa habari kuwa waangalifu
wanaporipoti habari za uchaguzi kwa kuhakikisha hazina upendeleo na kuepuka
kupotosha ukweli. Pia, amesisitiza umuhimu wa kutoa muda sawa kwa wagombea
wote.
Ameeleza kuwa mikutano hiyo
imeanzishwa na TCRA kwa lengo la kukuza sekta ya utangazaji nchini.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni:
"Wajibu wa Vyombo vya Utangazaji Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025."
0 Comments